July 6, 2016Na Saleh Ally
ACHA nianze na kukumbusha kidogo kwamba, msimu mmoja kabla ya uliopita, Juma Mwambusi alikuwa Kocha Mkuu wa Mbeya City ambaye ni timu inayomilikiwa na Manispaa ya Jiji la Mbeya.

 Alipoipandisha daraja msimu wa kwanza, moja kwa moja ikamaliza ligi ikiwa katika nafasi ya tatu, nyuma ya mabingwa Azam FC na Yanga walioshika nafasi ya pili, huo ulikuwa msimu wa 2013-14.

Msimu wa 2014-15, chini ya Mwambusi, Mbeya City ikamaliza ikiwa katika nafasi ya nne, baadaye kukawa na figisu zilizosababisha yeye kutangaza kuachana na klabu hiyo hadi uongozi ulipokaa naye chini na kuweka kambo sawa.


Ulipowadia msimu wa 2015-16 ambao sasa tunasema ni msimu uliopita, Mwambusi aliamua kuondoka Mbeya City na kujiunga na Yanga ambao ni mabingwa watetezi na walimtaka baada ya Kocha Charles Boniface Mkwasa kupewa jukumu la kuinoa timu ya taifa, Taifa Stars.

Wakati Mwambusi anatua Yanga, wengi sana walionekana kushangazwa au kutokubaliana na hali hiyo hasa wakitoa kigezo kwamba alikuwa kocha mkuu, sasa kaamua kujishusha ambalo si jambo zuri.

Wapo waliosema amejidhalilisha na wengine walipinga kabisa. Mimi nilisisitiza suala la kumpa nafasi kwa mambo mawili, maslahi lakini kujifunza kwa kuwa wote tunakubali kwamba hata kama Yanga na Mbeya City ziko ‘level’ moja kwa maana ya ligi, lakini Kocha Hans van Der Pluijm ni mwenye kiwango cha juu zaidi ya Mwambusi.

Kama Mwambusi alifuata maslahi pia ana haki, lakini leo niangalie upande wa mafanikio kwa maana ya mafunzo na kuongeza ujuzi alioupata kwa msimu mmoja akiwa na Yanga na namna gani angeukosa kama angebaki na Mbeya City.


 Yanga inafuzu kucheza Kombe la Shirikisho hatua ya makundi, Mwambusi ana mchango wake na amepata mafunzo mengi sana kwa vitendo huenda asingeyapata hata kidogo hata kama angeenda kusoma Ulaya.


Wakati mwingine masomo ya vitendo ni bora zaidi kwa asilimia ya uelewa au ubora wa kujenga kiwango cha ufahamu, kuliko yale ya maandishi pekee.

 Angepabaki Mbeya City angejua vipi namna timu za Waarabu zinavyopambana? Angejua vipi kuhusu fitna za Waangola? Angewezaje kujua kuhusiana na ugumu wa kupambana na timu kama TP Mazembe?

Hakuna anayeweza kukataa tena kwamba Mwambusi anaendelea kuzoa ujuzi kutoka kwa Pluijm ambaye anafanya naye kazi karibu kila siku ya wiki, tena kwa vitendo.


Mwambusi anazidi kukomaa kutokana na ugumu wa kazi ya kuifundisha timu inayoshiriki Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (Tanzania) na michuano ya kimataifa yaani Kombe la Shirikisho (Afrika).
Faida ambayo atakuwa ameipata Mwambusi hata kama maslahi ni kubwa pia, lakini mafunzo amepata makubwa ambayo ikifikia siku akipata timu na kuwa kocha mkuu, basi atakuwa mwingine kabisa na si yule Mwambusi wa Mbeya City.

 Bila ubishi, Mwambusi wa sasa, si yule wa Mbeya City kwa kuwa kuna vitu amepata, amejifunza na anaweza kuvitumia kwa faida ya kazi yake hapo baadaye.

 Alichofanya Mwambusi ni kuthubutu, jambo ambalo Watanzania wengi hata katika maisha ya kawaida hatuna, tunalihofia au si watu tulio tayari kupokea misukosuko.

Huwezi kupiga hatua kama haujaribu, kama muoga wa kupambana na misukosuko na mwenye hofu ya kukosolewa. 


Kila unapokosea ndiyo unajifunza ndiyo maana sasa ninasema, Mwambusi amefaidika na uamuzi wake wa kwenda Yanga ingawa alionekana anashuka cheo. Basi, tumpongeze na kujifunza pia kupitia kwake kwamba, kung’ang’ania mazoea na kuacha hofu itawale njia ya maisha yetu ni kujidumaza.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV