Ile sekeseke kati ya klabu ya Yanga na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusiana na suala la mapato, jana liliendelea na kuzua tafrani kubwa.
Ishu hiyo ilizuka mara baada ya mechi kati ya Yanga dhidi ya Medeama kwisha kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Baada ya hapo, fedha zilihesabiwa na lilipofikia suala la mgawo, uongozi wa Yanga ulikubali lakini kwa sharti moja, kutoa hundi na si fedha taslimu.
Yanga walisema wameamua fedha zote ziende benki na usiku huo wangezikabidhi kwenye kampuni ya ulinzi, kesho zingepelekwa benki na baada ya hapo, mgawo ungepitia mfumo wa hundi.
Kwa kuwa hilo halijazoeleka, TFF iliendelea kusisitiza kwamba watu wapewe mgawo wao "cash cash" kama ilivyozoeleka, Yanga wakashikilia msimamo wao.
Suala hilo baadaye liliamuliwa na Serikali na inaelezwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alitaka zisigawiwe ili kuwe na utaratibu sahihi.
Hali hiyo ilisitisha malumbano lakini inaonekana TFF ilikwazika kupita kiasi kutokana na Yanga kuanzisha utaratibu huo.
Lakini upande wa Yanga, ulijieleza kwamba umepanga kufanya hivyo ili kutumia mashine za EFD wakati wa malipo na itatoa lisiti kwa kila watakaolipwa.
Kabla ya mechi ya Medeama, kulikuwa na tafrani kubwa kati ya TFF na Yanga baada ya klabu hiyo kuruhusu mashabiki kuingia bure katika mechi ya TP Mazembe.
TFF iliambulia patupu, hali iliyofanya kuandika barua kadhaa ikidai ilipwe huku ikikadiria idadi ya watu uwanjani, jambo ambalo halikuwezekana.
0 COMMENTS:
Post a Comment