August 19, 2016Baada ya Yanga kukosa nafasi ya kufuzu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, kocha mkuu wa timu hiyo, Hans van Der Pluijm, amelitupia lawama Shirikisho la Soka Afrika (Caf) akidai kuwa kilichotokea ni sawa na upangwaji wa matokeo. 


Kocha huyo raia wa Uholanzi amedai kuwa matokeo katika mchezo wa Medeama dhidi ya TP Mazembe ambayo ndiyo yaliyoamua hatima ya Yanga katika michuano hiyo, yalikuwa na tatizo kwa kuwa kuna bao ambalo yeye binafsi anaona halikuwa halali.

TP Mazembe ya DR Congo tayari imeshafuzu hatua ya nusu fainali kutoka katika Kundi A ikiwa na pointi 10,  inafuatiwa na Medeama ambayo ina pointi nane wakati MO Bejaia ikiwa katika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi tano.

Yanga inaburuza mkia katika kundi hilo ikiwa na pointi nne na timu zote zimesaliwa na mchezo mmoja.

Kwa uhalisia Mazembe imeshajihakikishia kusonga mbele, huku timu mbili zinazofuata zikiwa na nafasi pia ya kusonga mbele, japokuwa Medeama inahitaji pointi moja tu ili ijihakikishie kusonga mbele pia.
Katika mchezo huo ambao Pluijm anaulalamikia, Medeama ilishinda mabao 4-3 dhidi ya TP Mazembe wikiendi iliyopita nchini Ghana ambapo bao la ushindi la timu hiyo lilifungwa dakika ya 90.
  
Akizungumza na Championi Ijumaa, Pluijm alisema kuwa  kamwe hawezi kukubaliana na ushindi wa Medeama kutokana na bao la ushindi katika mchezo wao dhidi ya TP Mazembe kuwa ni la ‘offside’ ya wazi isiyokuwa na kificho.

“Niliangalia mechi ya Medeama na TP Mazembe lakini kiukweli sijakubaliana na ushindi wao kwa sababu bao lao la ushindi mfungaji alikuwa ameotea bila ya kificho na kwa mtazamo wangu, mechi yao ilipaswa ichezwe siku moja na muda mmoja na ile yetu dhidi ya MO Bejaia.

“Kilichofanyika siyo haki kabisa, Medeama na TP Mazembe wameharibu matokeo yetu na hili ni kosa kubwa lililofanywa na Caf kuwaruhusu wao wacheze kwa siku moja mbele baada yetu, kitu ambacho siyo kizuri kwa maendeleo ya soka,” alisema Pluijm.

SOURCE: CHAMPIONI

3 COMMENTS:

  1. Mtakalia hayo hayo, kwani ninyi Yanga mlikatazwa kushinda mechi zenu? Timu zetu hazina uwezo wa kushindana Kimataifa,tutaendelea kuwa wasindikizaji na wenye uwezo wataendelea kuwa washindani.

    ReplyDelete
  2. Mtakalia hayo hayo, kwani ninyi Yanga mlikatazwa kushinda mechi zenu? Timu zetu hazina uwezo wa kushindana Kimataifa,tutaendelea kuwa wasindikizaji na wenye uwezo wataendelea kuwa washindani.

    ReplyDelete
  3. Mzee kavurugwa, kwa hyo unataka kusemaje? Kata rufaa sasa. Ulishindwa kutafuta ushindi mapema, unata Tp mazembe ndo akubebe? Upuuzi na ujinga mtupu

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV