August 19, 2016Na Saleh Ally, Barcelona
TAARIFA za Jamal Malinzi kufanikiwa kutetea nafasi yake ya uenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Kagera (KRFA), nimezipokea kwa masikitiko makubwa na imenishangaza sana.

Malinzi ameamua kugombea kwa mara nyingine kuwa Mwenyekiti wa KRFA na ameshinda. Sasa anaendelea kuwa na cheo hicho na rais wa TFF, hili ni jambo la ajabu kabisa.

Malinzi amegombea nafasi hiyo na kushinda, ameamua kufanya hivyo kwa kuwa tu katiba haimkatazi, kwake ni sawa kufanya hivyo!

Ninachojua katiba pia inatungwa na wanadamu na inawezekana ingetolewa mifano mingi sana kulilinda hilo, ‘yaani si unajua hata nanihii, au hata Ulaya au kule Fifa' na kadhalika.
Hata iwe vipi, kwa mtazamo wangu mimi naona ni jambo ambalo haliwezekani na hakuna kinachokwepeka kama utazungumzia suala la kubabaisha mambo kama tutaruhusu hilo.
Rais wa TFF ambaye ni bosi wa mikoa yote, ndiye bosi wa Mkoa wa Kagera. Maana yake huyu Malinzi ni bosi hadi kwake mwenyewe!

Ukitaka kusahau machungu ya mchezo wa soka unavyosuasua, hili nalo ni sehemu ya kuchekesha.
Katika soka nchini, kila siku vichekesho vipya. Kama ambavyo uliona, baada ya Azam FC kuitwanga Yanga na kubeba Ngao ya Jamii, wakati wakikabidhiwa pale uwanjani, dakika chache tu ikabanduka na kubaki kioo cha jamii. Mambo ndani ya TFF yanakwenda tu, raha tu na hakuna matata!

Huenda ndiyo maana jambo kama hilo la Malinzi kuwa rais na ‘mkuu wa mkoa’ linaonekana ni la kawaida sana. Binafsi naliona si sawa kwa mambo mengi sana.

Moja ninaamini Kagera kuna watu wengi sana wenye uwezo wa kuongoza, pili naona Malinzi ana majukumu mengi unapozungumzia maendeleo ya kisoka nchini, timu za taifa za watoto, vijana, wanawake na kubwa. Vipi anaweza kukaa akatulia na kufanya vitu vya Kagera.

Utaniambia vipi Malinzi anaweza kutenda haki kwa asilimia mia linapotokea suala la kuchagua kupeleka nyasi bandia kati ya Bukoba na Songea, au Kaitaba na Nangwanda Sijaona. Lazima atachagua sehemu ambayo yeye ni kiongozi mara mbili.

Hii si picha nzuri kwa kiongozi hasa ambaye yuko kwenye mpira kwa ajili ya maendeleo. Sidhani pia kama ni sahihi kufanya hivyo eti kwa kigezo kwamba katiba haikatazi au hata kule Fifa yupo nani hii anafanya kama hivyo.

Soka la Tanzania ni kimeo, viongozi wamekuwa chanzo. Kama kweli Malinzi anaamua kuingia huko, bado ni vizuri akajipa muda na nafasi ya kufanya mambo kuliko kujiongezea majukumu ambayo kuna watu wengi wangeweza kuingia na kusaidiana naye.

Kwenye uchaguzi mkuu inakuwaje, anajipigia kura? Lakini kwake faida ni ipi, anabaki na hiyo ili kujihakikishia kura? Au ni kweli kwa ajili ya maendeleo?

Soka ya Tanzania ina mengi imefeli, kunatakiwa juhudi za dhati kuiinua. TFF ya Malinzi nayo imeyumba, hata kuitetea inakuwa ni kazi kubwa kwa kuwa haina mwendo balansi, inayumba kila kukicha na hakuna kauli dhabiti kwenye mambo mengi ya msingi.

Ahadi tele, hakuna utekelezaji. Mipango mingi iliyojaa hadithi, migogoro isiyoisha na klabu utafikiri nayo inamiliki klabu. Sasa kiongozi wake mkuu, kuwa pia kiongozi wa mkoa ni jambo jingine la kuchekesha.

Ninaamini Malinzi ni mtu anayepapenda kwao Kagera kama ilivyo kwa wengine lakini hili la kuwa kiongozi wa mkoa na rais wa Shirikisho, si sura sahihi katika maendeleo ya mpira.

Binafsi naona ni kama hakuna malengo ya dhati kimaendeleo zaidi ya kuangalia upatikanaji wa sehemu au nafasi za uongozi na inawezekana isiwe kwa maendeleo ya mpira nchini.

Naiachia hapa, lakini ushauri wangu, ndugu yangu Malinzi aliangalie hili mara mbili kama kweli ana nia ya kusaidia mpira nchini, la sivyo hofu yangu kwake, itazidi hata mashaka kidogo niliyonayo. 


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV