August 20, 2016
MNAOBEZA uwezo wa mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa sikieni hii! Beki wa kimataifa wa Zimbabwe anayeichezea Azam FC, Bruce Kangwa, ameweka wazi kuwa mshambuliaji huyo ni hatari kutokana na kuwa na uwezo wa hali ya juu, tofauti na watu wanavyomchukulia.

Chirwa aliyesajiliwa Yanga kwa dola laki moja (zaidi ya Sh milioni 200 za Kitanzania) akitokea FC Platinum ya Zimbabwe, amekuwa kwenye wakati mgumu kutokana na kuonyesha kiwango cha kawaida kwenye michezo mbalimbali ya timu hiyo na mpaka sasa hajaifungia bao lolote licha ya kupewa nafasi mara kwa mara.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Kangwa anayecheza nafasi ya beki ya kushoto, amesema anamjua Chirwa kuwa ni mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa na kama akipewa muda zaidi, anaweza kuibeba timu hiyo kwenye michezo ijayo.
“Namjua Chirwa kwa sababu tumecheza wote kule Zimbabwe na ni mshambuliaji hatari, pia ni msumbufu kwa mabeki tofauti na watu wanavyomchukulia.
“Siamini kama ameshindwa kuonyesha kiwango kwa sababu hana uwezo, nadhani labda bado anaendelea kuzoea mazingira ya hapa na kama akipewa muda zaidi, basi watakuja kumkoma kwenye michezo ijayo,” alisema Kangwa ambaye ametokea timu ya Highlander ya Zimbabwe.

Mavugo azua hofu Simba, kocha apagawa
Sweetbert Lukonge
KIVUMBI cha Ligi Kuu Bara msimu wa 2016/17 kinaanza kutimua vumbi leo katika viwanja vitano tofauti kwa timu 10 kushuka uwanjani kuianza safari ya zaidi ya miezi nane ya kuwania ubingwa wa ligi hiyo ambao msimu uliopita ulinyakuliwa na Yanga.

Mechi hizo tano za ufunguzi wa ligi hiyo zitakazopigwa leo hii ni ile ya Simba dhidi ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Stand United na Mbao FC (Kambarage, Shinyanga), Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting (Manungu, Morogoro), Azam FC na African Lyon (Azam Complex, Chamazi) pamoja na Majimaji dhidi ya Prisons (Majimaji, Songea).

Simba ambayo imesajili wachezaji 11 msimu huu, watano wakiwa ni wa kimataifa na sita wazawa, macho na masikio ya mashabiki wake yatakuwa juu ya Mrundi, Laudit Mavugo ambaye amejiunga nayo hivi karibuni akitokea Vital’O.

Kwa upande wa Azam FC, mashabiki wake pia watakuwa wakiifuatilia mechi yake hiyo dhidi ya African Lyon iliyopanda daraja msimu uliopita wakitaka kuona ni jinsi gani imejipanga kuhakikisha inatwaa ubingwa wa ligi hiyo kwa mara ya pili tangu kuanzishwa kwake.
Hata hivyo, Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, ameliambia gazeti hili kuwa, kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mchezo huo pamoja na mingine yote inayokuja.

“Tupo tayari kwa ajili ya mechi hiyo na kila mchezaji yupo tayari kwa vita ili kuhakikisha msimu huu tunakuwa mabingwa. Wachezaji wa kimataifa ninaweza kuwakosa kutokana na kutokuwa na vibali vya uhamisho wa kimataifa (ITC) pamoja na vile vya kufanya kazi hapa nchini.

“Wachezaji ambao ITC zao hazijafika ni Besala Bokungu, Blagnon Fredric na Method Mwanjale lakini Mavugo na Mousa Ndusha wao ITC zao tayari tumeshazipata.

“Hata hivyo nina hofu kuwa ninaweza kuwakosa katika mechi hiyo kutokana na kutokuwa na vibali vya kufanya kazi hapa nchini kwani taarifa nilizopewa ni kwamba TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) imeagizwa na idara ya uhamiaji hapa nchini kuhakikisha kila mchezaji wa kimataifa anakuwa na kibali hicho ndipo aweze kuitumikia timu yake, vinginevyo hawatacheza,” alisema Omog.

Alipotafutwa Msemaji wa Simba, Haji Manara kuzungumzia suala hilo, alisema kila kitu kimeshakamilika juu ya wachezaji hao wa kimataifa isipokuwa Bokungu ambaye naye alikuwa katika hatua za mwisho kupata kila nyaraka inayohusika ili apate nafasi ya kucheza.

Rais wa Simba, Evans Aveva hakupatikana kwa kuwa simu yake ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa huku Katibu Mkuu, Patrick Kahemele akiwa hapatikana.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, alipoulizwa juu ya suala hilo alisema: “Nipo Nairobi, natokea Burundi kufuatilia ITC ya Mavugo ambayo tayari imeshafika, kwa hiyo mambo mengine yanayohusiana na uhamiaji sina taarifa nayo, waulize viongozi walioko huko.”

Mapema jana, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, alisema kuwa watu wa uhamiaji walifika katika ofisi za shirikisho hilo Ilala jijini Dar, juzi na kuwaagiza kuwa wachezaji wote wa kimataifa watakaoingia uwanjani wanatakiwa kuwa na vibali vya kufanyia kazi nchini, ikiwa vinginevyo basi mzigo utaiangukia TFF.

Alfred aliongeza kuwa klabu zote zinatakiwa kuwalipia wachezaji hao ada za leseni ambayo ni Sh 500,000 kwa kila mchezaji.

CHANZO: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV