KAMATI ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imemruhusu beki mpya wa Yanga, Hassan Kessy kuichezea timu hiyo msimu ujao wa Ligi Kuu Bara huku timu yake ya zamani ya Simba ikilalamika kuwa imeonewa.
Kessy, hivi karibuni alishindwa kuitumikia Yanga kutokana na Simba kugoma kutoa barua ya kumuidhinisha beki huyo kukipiga Jangwani kwa madai kuwa alikiuka makubaliano kwa kusaini mkataba mwingine kabla ya aliokuwa nao kumalizika huku ikitaka kulipwa dola 60,000 (sawa na shilingi milioni 126).
Beki huyo, juzi Jumatano alikuwepo kwenye kikosi cha kwanza kilichovaana na Azam FC kwenye mechi ya Ngao ya Jamii baada ya kamati hiyo kumruhusu kucheza mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Taifa.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema kamati hiyo iliyokuwa chini ya mwenyekiti wake, Wakili Richard Sinamtwa ilimruhusu kuichezea Yanga kwa makubaliano maalum.
Lucas alisema, kwa mujibu wa kamati hiyo, Simba imeomba ilipwe fedha hizo baada ya beki huyo kukiuka makubaliano yaliyokuwepo kwenye mkataba kutokana na kusaini Yanga akiwa ana mkataba.
Aliongeza kuwa, Simba inadai kuwa katika mkataba huo yalikuwepo makubaliano ya mmojawapo kati ya klabu au mchezaji akivunja mkataba, basi aliyevunja mkataba ni lazima amlipe mwenzake dola 60,000 ambazo Kessy anatakiwa kuzilipa.
“Suala la mchezaji Hassan Kessy limeegemea kwenye madai na si usajili ambako Simba ndiye mdai kwa kumtuhumu mchezaji huyo kuwa alianza kuitumikia Yanga kabla ya kumaliza mkataba wake. Mkataba wake ulifika mwisho, Juni 15, 2016.
“Kama ni madai Simba inaweza kuendelea kumdai Kessy au Yanga wakati mchezaji huyo anatumika uwanjani kwa mwajiri mpya. TFF inafuatilia na kuangalia haki ya Simba namna ya kupata haki yake baada ya kuwasilisha madai kuhusu kuvunja mkataba na mwajiri wake wa zamani.
“Kanuni hazimzuii mchezaji kuendelea kucheza kwa hoja ya madai badala yake suala hilo linaweza kumalizwa wakati mashindano yanaendelea. Kamati inaendelea kupitia malalamiko na pingamizi za wachezaji wengine na inatarajiwa kutoa taarifa rasmi kuhusu wachezaji wote wakati wowote kuanzia sasa,” alisema Alfred.
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit kuzungumzia hilo, alisema: “Hizo taarifa za kutakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha hatuna, kingine tunaomba ifahamike kuwa, Kessy tulimsajili Yanga kama mchezaji huru mara baada ya mkataba wake na Simba kumalizika, sasa tunashindwa kuelewa hayo mengine yanatoka wapi!”
Kwa upande wa meneja wa mchezaji huyo, Athumani Tippo, alisema: “Nashangazwa na taarifa hizo mpya kutoka kwako, mkataba wa Kessy na Simba ulimalizika tangu Juni 17 na akasaini Yanga, Juni 21, baada ya mazungumzo ya awali kufanyika mwishoni mwa Mei, hayo mengine sasa yanatoka wapi?”
Alipotafutwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Simba, Haji Manara, kuzungumzia hilo alisema: “Hayo maamuzi ya TFF kumuachia Kessy ni ya kutuonea, Kessy alisaini mkataba wa kuichezea Yanga akiwa bado ana mkataba na Simba, sasa iweje TFF imruhusu beki huyo kuichezea timu hiyo?”
CHANZO: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment