September 21, 2016


Timu ya Simba imeomba kurejesha mechi zake zote za Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa kutoka wa Uhuru jijini Dar es Salaam ili kuwaepusha wachezaji wake na majeraha.

Hiyo, ni siku chache tangu timu hiyo ichukue pointi tatu mbele ya Azam FC katika mechi ya ligi kuu iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, mechi iliyomalizika kwa Simba kushinda bao 1-0, lililofungwa na Shiza Kichuya.

Timu hiyo, hadi sasa imecheza michezo miwili ya ligi kuu kwenye uwanja huo tangu ilipohamishwa hapo kutoka Uwanja wa Taifa.

Katibu Mkuu wa timu hiyo, Patrick Kahemele alisema tayari wamemkabidhi barua Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura kuomba kurejesha michezo yao ya ligi kuu kwenye Uwanja wa Taifa kutokana na usalama wa afya za wachezaji wao.

Kahemele alisema, plastiki za kushika nyasi bandia za uwanja huo zimekauka, hali inayowapa hofu idadi ya majeruhi kuongezeka hapo baadaye, hiyo ni baada ya wachezaji wao watatu kupata majeraha kwenye mchezo uliopita na Azam.

 “Kiukweli usalama wa afya za wachezaji utaendelea kuwa mbaya kama tukiendelea kuutumia Uwanja wa Uhuru, kwani plastiki la kushika nyasi bandia limekauka, hivyo kuhatarishi afya za wachezaji wetu.

“Tayari tumeanza kupata majeruhi kwa wachezaji wetu kuchubuka ngozi chini ya unyayo wao kutokana vipira vya kwenye nyasi bandia pale uwanjani kuharibika kutokana na kutotumika kwa muda mrefu.

“Vipira hivyo, vimepigwa jua, vimefubaa hivyo kuhatarisha usalama wa wachezaji wanapoanguka chini, hivyo kiafya ni hatari kwao, hadi hivi sasa wachezaji watatu ni majeruhi waliyoyapata mara baada ya mechi na Azam,”alisema Kahemele.

Hata hivyo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana lilisema kuwa pia timu za Azam na Yanga nazo zilipeleka malalamiko kwao na hiyo wanataka kuchunguza hali hiyo na kuwasilisha malalamiko hayo kwa Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo.

SOURCE: CHAMPIONI0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV