September 21, 2016



Kwa mwendo iliyonao Simba ya sasa, ni wazi kwamba usitie mguu maana utavunjika tu! Hii ni kutokana na kasi ya ajabu iliyoanza nayo msimu huu, ikiwa ndiyo timu pekee iliyokusanya pointi nyingi zaidi katika mechi tano za mwanzo.

Simba iko kileleni na pointi 13, ikiwa imedondosha pointi mbili tu huku Azam FC na Yanga zikifuatia kwa pointi 10 kila moja, lakini Yanga ina mchezo mkononi.

Hata hivyo, Simba imefichua sababu kuu nne ambazo zimeifikisha hapo, ambazo inasema ndizo hizohizo zitakazoiua Yanga wiki ijayo kama ilivyokuwa kwa Azam wikiendi iliyopita walipoichapa bao 1-0.

Kabla ya hapo, tayari walikuwa wameshinda mechi dhidi ya Ndanda, Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar huku wakitoa suluhu na maafande wa JKT Ruvu.

Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja ‘Mia Mia’ ametamba kasi yao ni hiyohiyo kwa mechi zinazokuja ikiwemo ya Oktoba Mosi mwaka huu dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga kwenye Uwanja wa Taifa. 

Mayanja ambaye mara nyingi hutumwa na mkuu wake wa kazi, Joseph Omog ametaja sababu hizo kuwa ni pamoja na;

Ushirikiano, maelewano baina yao
Akitaja moja ya siri ya mafanikio mpaka sasa, Mayanja alisema ni ushirikiano mkubwa na maelewano mazuri kuanzia ngazi ya juu ya uongozi mpaka kwa mchezaji na mchezaji, hivyo kuwarahishia kazi wao kama wakuu wa benchi la ufundi kufanya kazi kwa ufanisi wa hali juu.

Kauli mbiu yao
Mayanja anasema mikakati ya benchi lao la ufundi ambayo wameigeuza kuwa kama kauli mbiu ni ‘kila mechi ni fainali, hakuna timu ndogo wala kubwa’, ambayo kwa kiasi kikubwa imewajengea moyo wa kupigana kila mechi.

Akitolea mfano mchezo na Majimaji ni sawa na Yanga wala Azam kutokana na ugumu wa ligi kwa ujumla.

 “Tumesema hakutakuwa na mechi ndogo wala kubwa, kila mchezo tunapoingia uwanjani, lazima tucheze kama mchezo wa fainali. Haijalishi ni timu gani wala mahali gani. Mchezo na Majimaji tunaupa hadhi sawa na huu (dhidi ya Azam) ama timu yoyote ile.”

Uhuru wa kufanya kazi
Kocha huyo wa zamani wa Kagera Sugar na Kiyovu Sport ya Rwanda amelidokeza kuwa uhuru wa kufanya mambo bila kuingiliwa na uongozi pia umechangia kikosi chao kufanya vema mpaka sasa, kwani kila kitu ni maamuzi yao kama benchi.

“Muhimu kila mmoja anafanya kazi yake, ushirikiano uliyopo baina yetu na viongozi kutimiza majukumu yao umesaidia sana. Kila kitu kinachohusiana na timu ni la benchi la ufundi na ndiyo maana wachezaji wanacheza kwa ari kubwa na kwa kuelewana zaidi.”

Ratiba kuwabeba:
Simba itacheza mechi saba mfululizo kwenye uwanja wake wa nyumbani, kati ya hizo tayari tano imezitumia vema kwa kushinda nne na sare moja na Mayanja amekiri ratiba kuwapa motisha zaidi.

Amekwenda mbali na kusema kuwa ‘tageti’ yao siyo hizo saba tu, wamedhamiria kuhakikisha kila mechi wanashinda.

“Kuna faida yake kucheza kwenye uwanja wa nyumbani kwa sababu hii inasaidia zaidi wachezaji kuzoea uwanja wenyewe kwa kuwa ndipo tutakuwa na mechi nyingi.

“Lakini kikubwa zaidi ni nyinyi wenyewe kuangalia jinsi ya kuzitumia. Tageti siyo hizo saba tu, tunapigana kuhakikisha kila mechi tunapata pointi tatu haijalishi tuko kwetu wala nje ya hapo, muhimu ni kutafuta ushindi ili kutimiza malengo yetu.”


Mchezo wa mwisho katika mfululizo wa mechi zao saba, Simba itakipiga na watani wao wa jadi, Yanga Oktoba Mosi, mwaka huu kabla ya kwenda Mbeya ambapo itacheza mechi mbili dhidi ya Prisons na Mbeya City.

SOURCE: CHAMPIONI.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic