September 28, 2016


Wakati zikiwa zimesalia siku mbili pekee kutoka leo kabla ya mechi ya Yanga dhidi ya Simba, beki wa kushoto wa Wanajangwani, Haji Mwinyi, amesema kuwa kwa uzoefu alionao wa mechi za kimataifa mpaka sasa, kamwe hawezi kuwa na presha na Simba aliyoiita ni nyepesi zaidi msimu huu.

Mwinyi ameeleza zaidi kuwa, kutokana na mechi ngumu walizocheza kwenye michuano ya kimataifa ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) na kukutana na timu vigogo Afrika kama Al Ahly ya Misri, hawezi kuhofia Simba inayoongozwa na wachezaji kama Ibrahim Ajibu, Laudit Mavugo na Shiza Kichuya.

“Nani? Hao kina Ajibu ndiyo watutishe sisi, wakati tushacheza mechi nyingi kubwa kuliko hiyo ya Simba, tumekutana na watu wapo vizuri huko kwenye mechi za kimataifa, mtu unacheza mpaka na mastraika wa Al Ahly halafu leo uhofie hawa wa Simba?

“Huo mchezo utakuwa na hadhi na presha yake kwa kuwa ni mchezo wa watani wa jadi, lakini tofauti na hapo, Simba yenyewe naona ni ya kawaida tu msimu huu tofauti na kipindi kile kuna akina Kessy (Hassan),” alisema Mwinyi na kuongeza:

“Unajua watu wasipate shida na kuona Simba imeifunga Majimaji mabao 4-0. Sisi tulipocheza na Majimaji tuliwafunga 3-0 pale Uhuru, sasa tungecheza nao Uwanja wa Taifa kama walivyocheza Simba, tungewafunga hata sita wale (Majimaji), watu wasiwe na presha, watulie.”


Yanga na Simba zinatarajia kukutana katika mechi ya kwanza msimu huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, Jumamosi hii huku kukiwa na kumbukumbu ya Simba kufungwa nje ndani katika mechi mbili za msimu uliopita. Kila mechi walifungwa mabao 2-0.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV