September 28, 2016Kasi ya ushindi kwenye mechi za Ligi Kuu Bara wanayoendelea nayo Simba, imezua hofu kwenye  kambi ya Yanga waliyoweka huko Pemba kujiandaa na mchezo wa watani wa jadi utakaopigwa Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga iliingia kambini huko Pemba juzi Jumatatu mchana wakitokea Shinyanga kuvaana na Stand United, katika mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo ilimalizika kwa kufungwa bao 1-0.

Simba hadi hivi sasa imecheza michezo sita ikishinda mitano huku mmoja wakitoka suluhu na JKT Ruvu wakati Yanga yenyewe imecheza mitano ikishinda mitatu, ikitoa suluhu na Ndanda FC huku ikifungwa mmoja na Stand United.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano kutoka ndani ya kambi hiyo, hofu kubwa imetanda ya kupoteza mechi hiyo kutokana na mwenendo mzuri wa matokeo wanayoendelea kuyapata Simba.

Mtoa taarifa huyo alisema, presha imeongezeka zaidi mara baada ya kipigo walichokipata dhidi ya Stand United hali inayosababisha kuzuka hofu kubwa ya kufungwa katika mchezo huo.

"Tupo kambini Pemba, lakini presha imeongezeka kwa kiwango kikubwa kutokana na matokeo mazuri ya ushindi wanayoendelea kuyapata watani wetu Simba.

"Kiukweli kabisa, wachezaji wetu wanahitaji somo la saikolojia ili kurejesha morali ya timu iliyopotea baada ya kufungwa na Stand, tunajua siyo kazi rahisi lakini tutahakikisha tunafanikisha hilo.

"Uongozi umepanga kukutana na wachezaji siku moja kabla ya mechi kwa ajili ya kuzungumza nao na kikubwa kutuliza presha ya mechi hiyo ili tushinde na hilo linawezekana kutokana na ubora wa kikosi chetu,"alisema mtoa taarifa huyo.


Alipotafutwa Kocha Mkuu wa timu hiyo Mholanzi, Hans van Der Pluijm kuzungumzia hali hiyo, alisema kuwa: "Siku zote zinapokaribia mechi za watani wa jadi presha inakuwa kubwa kwenye timu kwa kuanzia viongozi, kocha hadi wachezaji, lakini nikwambie kitu tu, wao wenyewe wanatuogopa sisi.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV