September 24, 2016


Akiwa na presha ya pambano la watani wa jadi Simba na Yanga, bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Cheka juzi jioni alivamia mazoezi ya Simba ili kuhakikisha ubora wa timu hiyo.

Cheka ambaye ni shabiki mkubwa wa Simba, amefanya hivyo ikiwa ni siku chache kabla ya pambano la Simba na Yanga la Ligi Kuu Bara litakalochezwa Oktoba Mosi, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 

Bondia huyo alifika katika mazoezi ya timu hiyo saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Boko Beach Veteran akiwa na meneja wake, Juma Ndambile na kufuatilia kwa makini kile kilichokuwa kikifanyika.

Akiwa uwanjani hapo akifutilia mazoezi hayo, Cheka alishindwa kujizuia na kueleza matumaini ya timu yao kupata ushindi kwenye mchezo huo uliojaa upinzani mkubwa.

Cheka alisema, matumaini hayo ameyapata kutokana na usajili bora wa kikosi chao kinachoundwa na wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa na uzoefu.

“Msimu uliopita Yanga walitunyanyasa sana kwa maana ya kutufunga mara zote mbili tulizokutana nao, kiukweli binafsi nilikosa amani.

“Mbaya zaidi mdogo wangu Cosmas (Cheka) yeye ni Yanga ambaye amemuambukiza hadi mtoto wangu, sasa nimekuwa nikikosa amani pale tunapofungwa kutokana na majigambo yao.

“Ndiyo maana leo (juzi) nimefika mapema uwanjani kwa ajili ya kushuhudia mazoezi ya timu yangu ili nijiridhishe, lakini nina matumaini makubwa ya kuwafunga Yanga.

“Jeuri ya kuifunga Yanga inakuja kutokana na msimu huu Simba imefanya usajili mzuri wa washambuliaji wazuri kama akina Mavugo (Laudit) na Kichuya (Shiza),” alisema Cheka.
0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV