September 24, 2016


Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm, amesema bado tabia ya kukamiwa na kuchezewa kwa undava kwa timu yake inapokuwa nje ya Dar es Salaam inaendelea na ametamba kushinda mechi zake pamoja na hali hiyo.

Kwa muda mrefu, Pluijm, raia wa Uholanzi, amekuwa akilalamika kuhusu Yanga kukamiwa katika mechi zake za mikoani kwani pindi timu zinazowakamia zikikutana zenyewe ‘hulegezeana’.

Yanga imeshinda mechi tatu kati ya nne ilizocheza na kuvuna pointi 10 zinazowaweka kwenye nafasi ya pili, yaani tatu nyuma ya Simba wanaoongoza ligi. Hata hivyo, Simba imecheza mechi tano, zote jijini Dar es Salaam.

Hadi sasa Yanga imecheza mechi mbili nje ya Dar es Salaam kati ya nne ilizocheza na kesho Jumapili inacheza dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga.

Akizungumza Pluijm alisema: “Tumejipanga vilivyo, bahati mbaya siku hizi kila timu tunayokutana nayo hufanya kila linalowezekana kuhakikisha hatushindi lakini tunapambana.

“Ukikutana nao wanahakikisha wanacheza zaidi ya asilimia 95 ili watudhibiti, lakini nashukuru vijana wamekuwa wakipambana kwa juhudi zote na kupata matokeo mazuri.

“Lakini ukitazama mechi zao wanacheza kawaida tu kiasi cha kuona kama tukikutana nao tunaweza kuwafunga mabao mengi lakini hubadilika kila tunapokutana nao hasa nje ya Dar es Salaam,” alisema Pluijm.

“Pamoja na hali hii, tutahakikisha tunashinda mechi yetu na Stand United ili kujiweka katika mazingira mazuri kabla ya kucheza na Simba wiki ijayo jijini Dar es Salaam.”


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV