September 8, 2016


SIYO tu uwanjani, Yanga wanakimbiza kwa kila kitu katika soka la Tanzania na kama ukiwalinganisha na watani wao wa jadi Simba, utakuta Yanga wapo juu tu.

Kuna hoja mbili kubwa katikati ya hizi timu kongwe, kwa Yanga mwenyekiti Yusuf Manji yupo katika mchakato wa kuikodi nembo ya timu kwa miaka 10 wakati kwa upande wa Simba Mohammed Dewji ‘Mo’ anataka kununua hisa asilimia 51 za klabu hiyo kwa dau la Sh bilioni 20.

Hawa wote ni matajiri wenye fedha nyingi lakini Manji tayari ameshaipeleka Yanga kwenye ‘levo’ za kimataifa kutokana na mkwanja mrefu anaomwaga klabuni hapo, hivyo kama Mo akifanikiwa kupewa Simba atakuwa na mlima mrefu wa kupanda kufikia kile ambacho Manji anakifanya kwa Yanga hivi sasa.

Kabla hata hajaikodi Yanga, Manji ameonekana kumwaga fedha nyingi ambazo zinaosaidia Yanga kupata mafanikio na itamlazimu Mo amwage fedha nyingi sana ili kukifikia kile anachokifanya Manji kwa sasa. 

Championi Jumatatu limefanya tathmini ya ukubwa wa hizi timu kongwe na jinsi zinavyotumia fedha na kukuta Yanga inakimbiza katika kila idara.

Thamani ya kikosi:
Tathmini ya Championi Jumatatu kupitia vyanzo vyake vya uhakika, imebaini kuwa thamani ya kikosi kizima cha Yanga ni Sh 1,300,000,000 (Sh bilioni moja na milioni mia tatu). Hii inamaanisha fedha ambazo zimetumika kuwasajili wachezaji wote wa kikosi cha kwanza ilionao kwa ajili ya msimu huu wa Ligi Kuu Bara na michuano mingine.

Wakati thamani ya kikosi hicho cha Yanga ikiwa hivyo, upande wa pili, thamani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi ni Sh 1,003,275,000 (Sh bilioni moja na milioni tatu laki mbili na sabini na tano).
Hii ina maana kwamba kama ukilinganisha vikosi hivi viwili, utakutana na ukweli kwamba Simba inazidiwa kiasi cha Sh 296,725,000.

Malipo ya mishahara:
Malipo ya mishahara kwa mwezi ya wachezaji, benchi la ufundi na sekretarieti kwa Yanga jumla ni shilingi milioni 160, hii ni kwa mujibu wa tamko alilolitoa mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji wakati wa uchaguzi mkuu wa timu hiyo Juni 11, mwaka huu. Chanzo kimoja cha habari ndani ya Yanga kimeliambia gazeti hili kuwa katika kiasi hicho, kitita cha Sh milioni 120 hutolewa kila mwezi kwa ajili ya kuwalipa wachezaji tu na kinachobaki ndiyo wanagawana wengine.

Kwa upande wa Simba, malipo ya mishahara ya wachezaji, benchi la ufundi pamoja na sekretarieti ni Sh milioni 78 tu kwa mwezi, hiyo ni kwa mujibu wa chanzo chetu cha ndani ya Simba.

Ukilinganisha hapo utakuta Simba imefunikwa na Yanga kwa jumla ya kitita cha Sh milioni 82, yaani kila mwezi Yanga inatoa Sh milioni 82 zaidi ya kiasi inachotoa Simba.

Mchezaji mwenye thamani kubwa:
Nyota aliyesajiliwa kwa thamani kubwa zaidi ya wote katika kikosi cha Yanga ni Obrey Chirwa raia wa Zimbabwe ambaye alisajiliwa kwa Sh milioni 240, wakati kwa upande wa Simba mchezaji mwenye thamani kubwa zaidi ni Fredric Bragnon raia wa Ivory Coast aliyesajiliwa kwa Sh milioni 100. Hapo utaona Simba imefunikwa tena kwa zaidi ya Sh milioni 140.

Anayelipwa zaidi:
Wachezaji wanaolipwa zaidi kwa upande wa Yanga wamefungana watatu ambao ni Donald Ngoma, Chirwa, Thabani Kamusoko na Haruna Niyonzima ambao wanakomba kitita cha dola 3,500 (zaidi ya Sh milioni saba) kwa mwezi.

Kwa upande wa Simba mchezaji anayelipwa zaidi ni Blagnon na Laudit Mavugo raia wa Burundi ambao wamefungana kwa kulipwa dola 1,500 (zaidi ya Sh milioni tatu) kwa mwezi.

Ukilinganisha hapo utakuta Simba imepotezwa tena, kwani wachezaji wao wanaolipwa zaidi wapo chini kwa kiasi cha Sh milioni nne ukilinganisha na wale wa Yanga.

Mzawa anayelipwa zaidi:
Mchezaji mzawa anayelipwa zaidi Yanga anachukua Sh milioni 5 kwa mwezi ambaye ni Simon Msuva, wakati kwa upande wa Simba mzawa anayelipwa zaidi ni Jonas Mkude ambaye anapokea kitita cha Sh milioni mbili. Hapo utaona Yanga ipo mbele ya Simba kwa Sh milioni mbili.

Mashabiki:

Yanga inakadiriwa kuwa na mashabiki milioni 20 Tanzania nzima, hii ni kwa mujibu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Yanga, kwa upande wa Simba yenyewe inakadiriwa kuwa na mashabiki milioni 15 kwa mujibu wa hotuba ya rais wa klabu hiyo, Evans Aveva aliyoitoa katika mkutano mkuu wa dharura uliofanyika mwezi uliopita.

6 COMMENTS:

 1. Acha unazi, kichwa cha habari hakiendani na content ya kazi yako na pia hujatoa solution, kazi yako ni kuandika tofauti zilizopo ili upate kick. So what?

  ReplyDelete
 2. Mwandishi uchwara umeona bora ufute hoja yangu.Hata kama umefuta kile nilichokieleza bado mwangwi wake utaendelea kusikika kwenye kuta za moyo wako.Kuifuta hoja yangu kumedhihirisha jinsi ulivyo mnafiki kwenye hoja zako na usivyoweza kuukubari ukweli.Endelea kutumika na kulitumia Championi kuwa kipaza sauti cha yanga,soon Gazeti lako linalochochea chuki na migawanyiko kwa klabu shindani na yanga litaanza kupaukia kwenye mbao za wauza magazeti.

  ReplyDelete
 3. Naweza kusema ni kweli Yanga wanaizidi Simba kwa hivyo vitu lakini kumzidi mtu kwa matumizi si lazima iwe sifa nzuri. Kwa mfano tu nihoji Obrey Chirwa aliyesajiliwa kwa mil 240 anamzidi nini Mavugo, Ajibu au Msuva wa milioni chache. Je, kulipa mishahara mikubwa peke yake bila kigezo kingine ni sifa nzuri? HAPANA.
  Kikubwa nachopingana na wewe ni kuwa MO hana haja ya kushindana na Yanga kwenye hayo maeneo uliyoyataja ili afanikiwe Simba. Ana mipango yake tofauti (hasa ya uwekezaji) ambayo anaamini italipa na kuwezesha Simba Kujiendesha. Pamoja na Manji kumwaga hela Yanga haina hata uwanja wa Mazoezi, wala haijetegemei, na plan ya kuikodisha ikaja mbio mbio ili kushindana na Simba au MO (Huu ni utoto). MO hayuko hivyo na ndio maana husikii hata akigombana hovyo na watu (Maoni yangu).
  MO HANA HAJA WALA SABABU YA KUSHINDANA NA YANGA ILI AFANIKIWE SIMBA

  ReplyDelete
 4. Siamini km matumizi ya pesa ndio matokeo ya kufanya vzr uwanjani. Kucheza caf sio mafanikio ya kulingia maana Simba walishawahi kucheza hadi fainali ya confederation na nusu fainali. je kipindi hcho simba walikuwa na pesa zaidi. Hivi Leicester amawekeza pesa nyingi na ana matumizi makubwa ya pesa na washabiki wengi kuliko man u, man city, chelsea, arsenal kwa sababu wamefanya vzrr? au A.Madrid wamewekeza pesa nyingi kuliko Barcelona mcimu uliopita maana wamefanya vzr CL au misimu miwili iliyopita walipobeba La Liga walikuwa na wachezaji wanaolipwa pesa nyingi kuliko R.M na Barca?

  ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV