September 20, 2016




Kadi za kilektroniki kwa ajili ya kuingia uwanjani zitakuwa zikitolewa bure.

Hii ni ni baada ya ya hivi karibuni serikali kufunga mashine za kielektroniki katika Uwanja wa Taifa, kadi kwa ajili ya kuingilia uwanjani humo zitatolewa bure.

Serikali iliamua kufunga mashine hizo katika uwanja huo ili kuondokana na mfumo wa zamani wa kutumia tiketi za kawaida kwa lengo la kulinda mapato yake uwanjani hapo ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa yakiishia mifukoni mwa wajanja wachache.


Akizungumza katika semina elekezi ya jinsi ya kutumia mfumo huo mpya wa kuingia uwanjani humo uliozinduliwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, Meneja Miradi wa Kampuni ya Selcom ambayo ndiyo iliyopewa jukumu la kusimamia mfumo huo, Gallus Runyeta amesema kuwa kadi zitakazokuwa zikitumika katika mfumo huo zitatolewa bure.

Amesema kadi hizo zitaanza kutolewa hivi karibuni ambapo kutakuwa na mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaofanyika katika uwanja huo ambao serikali kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) watauandaa kabla ya mchezo wa Yanga na Simba.

“Kadi zinapatikana kwa mawakala wetu (wa Selcom) waliopo kila sehemu. Lazima ununue tiketi halafu unapewa kadi bure,” alisema Runyeta.

Akizungumzia jinsi ya kuitumia kadi hiyo, Runyeta amesema: “Utajisajili kwa kupiga *150*50# halafu ni lazima uiwekee pesa kwa Airtel au M-Pesa. Kiwango cha chini cha kuongeza salio ni Sh 1,000.

“Unaweza ukanunua mechi moja kwa kuandika tarehe na mchezo husika au ukachagua baadhi ya mechi au ukanunua mechi zote za msimu za timu unayoipenda.

“Unapokwenda kuingia uwanjani, utaweka kadi yako kwenye alama husika na mlango utafunguka wenyewe. Ukishaangalia mechi uliyoinunua, hauwezi kesho yake ukaenda kutazama mechi nyingine ambayo hujailipia. Kadi itasoma kwenye mechi zilizolipiwa tu. Ukiingia uwanjani hauwezi ukatoka halafu ukarudi kwa tiketi ileile. 

Tunawashauri watu wawe wananunua tiketi mapema ili kuepusha usumbufu na msongamano milangoni. Unaweza ukanunua siku nyingi kabla.”


Ameongeza: “Mbali na kadi hizo kuzitumia uwanjani, pia aliyenayo anaweza kuitumia kwa matumizi mengine kama vile kuhifadhi na kutoa fedha kwa wakala, lakini pia inamwezesha mtu huyo kulipia bidhaa na huduma mbalimbali bila kuwa na fedha mfukoni.”

Wakati huohuo, Nnauye amemuagiza Naibu Mkurugenzi wa Michezo Tanzania, Nkenyenge Alex kuhakikisha anaandaa sera ya michezo nchini mapema iwezekanavyo mpaka kufikia mwezi Septemba iwe tayari.

Amesema lengo kubwa la kufanya hivyo ni kutaka kuleta mapinduzi makubwa ya michezo hapa nchini kwani sera iliyopo hivi sasa imeshapitwa na wakati.

“Nimemwambia nataka mpaka kufikia Septemba sera hiyo iwe tayari, kama atashindwa kufanya hivyo, basi akatafute sehemu nyingine ya kufanya kazi pamoja na wenzake wote,” amesema Nnauye.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic