September 20, 2016



Na Saleh Ally
KIKOSI cha timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Queens, kimebeba kombe la Chalenji kwa mara ya kwanza na kuweka rekodi.

Timu ya taifa ya Tanzania Bara kwa wanawake imewachapa Wakenya kwa maabo 2-1 katika mechi ya fainali iliyochezwa Uganda na kubeba kombe hilo.

Rekodi yenyewe ni hii, kuwa wao ndiyo timu ya kwanza ya Ukanda wa Afrika Mashariki kubeba Kombe la Chalenji ambalo limefanyika kwa mara ya kwanza.

Kilimanjaro Queens, sawa, lakini kilikosi hicho kwa zaidi ya asilimia 90 ndiyo wale Twiga Stars ambao ni timu ya taifa ya Tanzania.

Akina dada ambao sasa wanaondoka kwenye sura za utoto, wamekuzwa na kufikishwa hapo na watu wengi sana waliojitolea.

nimeona pongezi nyingi zinakwenda kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ni jambo jema kwa kuwa mwishoni hapa wamejitolea kwa ajili yao.

Lakini nimeona niwakumbushe wadau kwamba mafanikio ya kikosi hicho, sifa nyingi ziwaendee waanzilishi wa Sayari FC, waanzilishi wa Mburahati Queens akiwemo Dk Tamba  na wengine walioanzisha timu za wanawake.

Pongezi zaidi kwa Chama cha Soka Kinondoni (KIfa) ambacho kilionyesha kuthamini soka la wanawake tokea mwanzo na viongozi wake kama Mchaki, walikuwa kiwapambana kwa muda mrefu.


Wakati wa TFF ya Leodeger Tenga, pia walionyesha kuijali timu ya taifa ya wanawake ambayo wachezaji wake wengi leo ndiyo wamechukua ubingwa huo wa Afrika Mashariki. Kama unakumbuka walivuka hatua kadhaa za michuano ya Afrika.

Wako wadau walijitokeza na kuonyesha upendo wao wa dhati na kuunga mkono uchezaji wa Twiga Stars na ligi ya wanake. Ninaamini wachezaji wa Twiga Stars wanaweza kusema mtu kama Dk Damas Ndumbaro alivyokuwa akijitolea na kuwapa moyo ikiwa ni pamoja na kuwanunulia vifaa wengine.

Twiga Stars inaing’oa Ethiopia kwao jijini Addis Ababa, Dk Ndumbaro alikuwa kati ya viongozi wa msafara uliokuwa jijini humo na hata baada ya mechi vijana walikimbia na kumkumbubatia kwa furaha wakionyesha kuthamini mchango wake.

Kwa sasa, Waziri Nape Nnauye ambaye ana dhamana ya michezo, ameonyesha uzalendo na ushiriki wake kwa karibu tofauti na awali ilivyokuwa kwa viongozi waliopita.

Huu ni uwakilishi mzuri wa serikali michezoni na unachagiza kwa kiasi kikubwa mafanikio hayo yanayojitokeza kwa sasa pia.

Akina dada wa Kili Queens, hakika hongera sana kwa kuibandua Kenya na kubeba Chalenji. Lakini bado mna safari ndefu kuendelea kuusukuma mchezo wa soka kwa wanawale na ukweli ni kwamba mlichofanya ni kuionyesha jamii kwamba mnaweza.

Maana yake, wadau wawape nafasi zaidi, wawathamini zaidi na kuwasukuma zaidi muendelee kufanya vema.

Kuna mtihani kwa Zanzibar, kikosi chao ni dhaifu sana. Huenda changamoto ya ushindi wenu inaweza kuwa sehemu ya chachu ya wao kubadilika pia kama watakuwa na hamu ya kubadilika na kupata mafanikio.

Hongera kwa kila mmoja aliyewahi kutoa mchango wake wa aina yoyote kuiunga Twiga Stars. Lakini bado safari haijafikia tamati.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic