September 5, 2016

SALEH ALLY AKIWA NDANI YA VYUMBA VYA KUBADILISHIA NGUO VYA REAL MADRID, KARIBU KABISA NA SEHEMU AMBAYO HUKAA CRISTIANO RONALDO. FUATILIA...

Na Saleh Ally aliyekuwa Madrid
UBORA wa kitu mara nyingi huchangiwa na watu wenye malengo ya kufanya vizuri au kufika mbali kutokana na wanachokifanya.

Klabu ya Real Madrid ya Hispania, imejijengea daraja na mambo yake mengi hivyo kuifanya iwe tajiri zaidi duniani kwa kuwa kila kitu chake ni bora zaidi.

Championi lilipata nafasi ya kuvinjari kwenye vyumba vya wachezaji wa kubadilishia nguo vya wachezaji wa Real Madrid kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu ulio katikati ya Jiji la Madrid ambalo ni kubwa zaidi na makao makuu ya Nchi ya Hispania.

Championi ni gazeti la michezo Tanzania lililopata nafasi ya kupita kwenye vyumba vingi zaidi vya timu za Ulaya. Vile vya Madrid, vinaonekana kuwa bora zaidi kutokana na mambo kadhaa.


Wasomaji wa Championi wanaweza kufaidika zaidi kutokana na kusoma na kujua namna vyumba hivyo vilivyo, namna timu hiyo tajiri ilivyoweka mambo yake tofauti. Mfano ni vyumba vya wachezaji wake ambavyo ndani ni kasoro vitanda vya kulala tu, lakini huduma yake, inazidi hoteli nyingi za kitalii!

Unapoingia kwenye vyumba vya Real Madrid, utagundua kitu cha kwanza wachezaji hukaa kwa namba kuanzia moja na kuendelea hadi 23, 24 na kadhalika. Kila mmoja nyuma ya kabati lake kunakuwa na picha yake kubwa akiwa na jezi ya Madrid pamoja na namba yake.

Ndani ya ile picha ni kabati maalum ambako anaweza kuhifadhi vitu vyake. Ndiyo maana wachezaji wakati wanaingia uwanjani utawaona wakiwa wamebeba mabegi yao madogo, ambayo yanakuwa na manukato ‘losheni’, vitana na kadhalika.


Wakiingia wanahifadhi kwenye kabati hizo na baada ya mechi, huoga na baada ya hapo hupaka au kupulizia wanachotaka kabla ya kuondoka.

Mfumo wa klabu za Hispania, kama zipo nyumbani, kila baada ya mechi, kambi huvunjwa rasmi hapo uwanjani na wachezaji huondoka na familia zao, siku inayofuata ni mapumziko.

Hivyo maandalizi ya mechi hufanyika na wachezaji wanapoingia vyumbani, kunakuwa na madaktari wawili ambao wanakuwa wanazunguka kujua kila kinachoendelea. Madaktari hao wana chumba chao ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo na kila baada ya mechi, kila mchezaji anayehitaji hufanyiwa masaji anafanyiwa.

Mchezaji anachagua kwa kuwa kuna nafasi ya kufanya masaji nyingine ya aina mbili baada ya ile ya madaktari. Iko ile ya kwenye Jacuzzi.

Hili Jacuzzi ni kama bwawa dogo la kuogelea lakini linakuwa na maji ya uvuguvugu ambayo huufanya mwili kupunguza makali ya uchovu baada ya mechi.


Jacuzzi hilo linaweza kuchukua hadi watu wanane, pia ni aghalabu sana kukuta kwenye chumba cha wachezaji kuwa na bwawa kama hilo.

Masaji ya aina ya tatu baada ya ile ya madaktari na Jacuzzi, ni ya chumba maalum kinachotoa maji yaliyo-‘setiwa’.

Unapofungua maji katika chumba hicho, unachotakiwa ni kuzunguka na kuacha yakupige kila sehemu na baada ya dakika 5 hadi 10, mwili unapunguza maumivu.

Hivyo utaona, wachezaji wa Real Madrid wanapokuwa vyumbani, wanakuwa utafikiri wapo kwenye hoteli ya kitalii na huduma yao inakuwa tofauti kabisa na wachezaji wa timu nyingine ikiwezekana karibu zote kwa asilimia 99.

Kwa mchezaji ambaye hataki masaji au kujipumzisha kwenye Jacuzzi, yeye anaweza kuoga kawaida kwa kutumia bafu ambalo ni maalum ambalo mtu anaoga akiwa amesimama.

Bafu hilo lililojengwa kwa malumalu za kifahari kabisa, lina uwezo wa kuchukua hadi wachezaji 11 kwa wakati mmoja na wengi huanzia hapo kuoga au hata kutoa jasho kabla ya kwenda kwenye upande wa masaji hiyo ya aina tatu tofauti.


Bafu hili pia hutumika zaidi wakati wa mapumziko kwa kuwa baadhi ya wachezaji hupendelea kujimwagia maji kidogo wanapoingia vyumbani dakika 5 za mwanzo wakati wa mapumziko, halafu wanabadilisha jezi kwa kuwa timu kubwa ikiwemo Madrid, kila mechi mchezaji hukabidhiwa jezi mbili, huku kukiwa na moja ya akiba ambazo zinabaki vyumbani chini ya msimamizi wa utoaji vifaa.

Ndiyo maana unaona, wachezaji mara baada ya kipenga cha mapumziko hukimbia kasi vyumbani maana dakika tano za mwanzo, zinakuwa ni mali yao. Baada ya hapo, kocha anakuwa na muda wake.

Hivyo lazima wautumie vizuri muda wao na kukaa ili kumsikiliza kocha, hapa unatakiwa kuuwahi muda, si mambo ya Kiswahili tena.

Kwenye bafu hilo, hakuna sabuni ya kipande, jiwe la kujisugulia au dodoki! Badala yake ni sabuni maalum ya maji ambayo inakuwa kwenye vifaa maalum. Hivyo mhusika anabonyeza tu inatoka, anajipaka na baada ya hapo ni kuoga. Hapo pia ana uwezo wa kuchagua anataka maji ya baridi, saizi ipi, uvuguvugu au moto.

Ndani ya vyumba hivyo, kocha pia anakuwa na sehemu yake maalum. Huku utaona nyota wa timu hiyo, Cristiano Ronaldo akiwa anakaa katikati ya Nacho ambaye anavaa namba 6 na Kroos ambaye huvaa namba 8.


Hispania, wanaamini vyumba vya kubadilishia nguo ni sehemu inayotakiwa kuwa bora, yenye mvuto na hali inayomhamasisha mchezaji kwenda kufanya kazi bora kwa ajili ya klabu inayoonyesha kumjali.


Ndiyo maana, hata pamoja na ubora wa vyumba hivyo vya wenyeji Madrid kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu, vile vya upande wa pili, yaani vya timu mgeni, vinabaki kuwa vya kawaida tu, ili kusaidia kumvuruga mgeni ili ‘apigwe tu’.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV