September 12, 2016

Katika mazoezi ya wiki iliyopita, Kocha wa Simba, Joseph Omog, alivalia njuga tatizo la ufungaji kwenye kikosi chake, zikiwemo mbinu mbadala za kupiga mashuti ya mbali na makali, pindi mbinu ya kufika kwenye boksi ikishindikana.

Hata hivyo, katika kipengele hicho cha mashuti, kiungo Said Ndemla ambaye amekuwa hana namba kikosi cha kwanza kwa muda mrefu, alionekana mwiba mkali kwa kuwafunika wakali wengine kama Jonas Mkude, Mousa Ndusha ambao pia ni hatari kwa mashuti makali. Wajerumani ndiyo wamekuwa na sifa ya kupiga mashuti makali, hasa kwenye ligi kuu ya nchini humo  (Bundesliga).

Said Ndemla

Katika mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa jana dhidi ya Mtibwa, Alhamisi na Ijumaa, Omog alionekana kukazania zaidi kutumia nafasi hata kama ni nje ya boksi kwa kuachia makombora makali.


Umati wa mashabiki uliishia kumshangilia kwa makofi Ndemla kwani asilimia kubwa mashuti yake yalitinga kambani huku makipa Peter Manyika, Vincent Angban wakiruka ‘kiushahidi’ tu pengine kutokana na uzito wa mashuti yenyewe.


Tayari Omog amempa nafasi ya kuanza katika mechi dhidi ya Ruvu Shooting baada ya kukosa nafasi kabisa wakati wa ‘utawala’ wa Mganda, Jackson Mayanja ‘Mia Mia’ msimu uliopita.


Alipoulizwa kuhusu kiwango chake, Ndemla alisema: “Bado tunapigana, ni mapema kuzungumzia nafasi hiyo lakini ngoja tupambane kwanza tuone baadaye.”



 

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic