September 12, 2016

Kocha wa Azam FC, Mhispania, Zeben Hernandez, ameweka bayana kwamba wana kila sababu ya kikosi chake kuibuka na ushindi mbele ya Simba wikiendi ijayo kwa sababu wana morali ya kutaka kushinda kwenye kila mchezo wao.

Zeben amefanikiwa kuiongoza Azam kukamata usukani wa ligi ikiwa na pointi 10 ambapo wikiendi hii itashuka dimbani kumenyana na Simba inayofundishwa na Mcameroon, Joseph Omog kwenye mchezo utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar.


Kocha huyo amelieleza gazeti hili kwamba ni lazima kikosi chake kiweze kushinda mchezo huo dhidi ya Simba kutokana na kutaka kufikia malengo yao ya kutwaa pointi kwenye kila mchezo wao.


“Tuko vizuri sana na wachezaji wana morali kubwa ya ushindi, hivyo naamini kwamba mchezo wetu ujao tutashinda licha ya kwamba haitakuwa rahisi kwa sababu wapinzani wetu nao wamejiandaa na wana kikosi imara kama chetu. 


“Ila kwetu ushindi ni muhimu kwa sababu malengo yetu kwenye kila mchezo ni kutaka pointi tatu bila ya kuangalia nani tunacheza naye kama ambavyo tulifanikiwa kuzipata tukiwa jijini Mbeya mbele ya Prisons na Mbeya City,” alisema Zeben.  

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV