September 17, 2016

Kocha wa Prisons, Meja Mstaafu, Abdul Mingange amesema anafahamu kila kitu cha wapinzani wake Mbeya City hivyo hawatamsumbua katika mchezo wao wa leo Jumamosi.

Prisons na Mbeya City, timu ambazo ni wapinzani wa jadi, zinakutana leo jioni katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya. Pambano hili pia hufahamika kama Mbeya Derby.

 

Mchezo huo unasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa timu hizo kwani mshindi anaweza kusogea juu katika msimamo wa ligi kwa kuwa zote zina pointi saba baada ya kucheza mechi nne.

Akizungumzia mchezo wa leo, Mingange alisema ana matumaini ya kushinda kwani anaijua vizuri Mbeya City kutokana na kuifundisha msimu uliopita.

“Unajua kwanza wao (Mbeya City) wanatujua vizuri na sisi tunawajua, kifupi tunajuana kwa sababu tunakaa pamoja halafu wameona mechi zetu ila hiyo haiwezi kunitisha,” alisema Mingange.


Kwa upande wake Kocha wa Mbeya City, Kinnah Phiri, raia wa Malawi, alisema: “Hii ni mechi ngumu kwa sababu ni ‘derby’ ambayo mara nyingi matokeo yake yanakuwa hayajulikani.


“Lakini siwezi kuhofia kwa sababu nawajua Prisons, wao wana tatizo la ushambuliaji ambalo pia lipo kwenye timu yangu, kwa sababu hakuna kati yetu ambaye ameweza kufunga mabao mengi.”

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV