September 17, 2016

Leo Jumamosi jioni nyasi za Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam zitawaka moto kwani Simba inacheza na Azam FC katika Ligi Kuu Bara, gumzo nyuma ya pazia ni posho zinazotolewa na bilionea Mohammed Dewji ‘Mo’.


Hivi karibuni uongozi wa Simba ulianzisha utaratibu wa kuwapa wachezaji wa timu hiyo Sh milioni 5 kila wanaposhinda mechi ya ligi kuu na kweli hilo limeonekana kufanikiwa.


Kweli fedha hizo zilikuwa hamasa ya Simba kuifunga Ruvu Shooting mabao 2-1 na Mtibwa Sugar mabao 2-0 baada ya awali kuifunga Ndanda FC mabao 3-1 na suluhu na JKT Ruvu.


Hali hiyo, pia ilimvutia bilionea Mo ambaye naye ameongeza Sh milioni 5 ambazo zitakwenda kwa benchi la ufundi kwa kila mechi ambazo Simba inashinda.


Hiyo ina maana, Simba ikishinda tu sasa inapata Sh milioni 10.


Chanzo chetu kutoka benchi la ufundi la Simba kilisema: “Kundi la kwanza ni lile la wachezaji ambao hupata nafasi ya kucheza, hawa hupewa Sh 400,000.


“Kundi la pili ni lile la wachezaji ambao walivaa jezi lakini hawakucheza, wao hupewa Sh 200,000 na kundi la tatu ni lile la wachezaji ambao wanakaa jukwaani, hao hupata Sh 100,000.


“Kwa hali hiyo, kila mchezaji atakayefanikiwa kucheza mechi nne kwa mwezi na zote wakashinda basi ana uhakika wa kupata Sh milioni 1.6, tena hizo ni nje ya mshahara.


“Kwa yule ambaye atakuwa akikaa benchi bila kucheza atakuwa akichukua Sh 800,000 na yule ambaye atakuwa jukwaani basi ataondoka na Sh 400,000 kwa mwezi.


 “Mbali na wachezaji lakini pia hata viongozi wa benchi la ufundi pamoja na madereva wanaowaendesha makocha na wachezaji pia hunufaika na fedha hizo.”


Katika zile Sh milioni 5 za kwanza, mgawo ulikuwa Sh 200,000 kwa wachezaji waliocheza, Sh 100,000 kwa waliovaa jezi bila kucheza na Sh 50,000 kwa wale wanaokaa jukwaani.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic