September 16, 2016

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Poppe ametoa kauli ambayo inaweza kuongeza moto kwa mapambano kwa wachezaji wake hasa wawili ambao amewataja majina.

Kiongozi huyo amewataja wachezaji Ibrahim Ajib na Jonas Mkude kuwa ameridhishwa na viwango vyao na yeyote kati yao atazawadiwa gari kama ilivyokuwa kwa beki wa timu hiyo, Mohammed Hussein Zimbwe ‘Tshabalala’, aliyepewa gari aina ya Toyota Raum baada ya kushinda kuwa mchezaji bora wa timu hiyo.
  Akizungumza na Championi Ijumaa, Poppe alisema wanatarajia kupata changamoto kubwa ya kumpata mshindi mwingine anayefuata wa gari kutokana na wachezaji kubadilika kwa kiasi kikubwa.

Alisema kwa upande wa Ajib, ameonekana kujitambua hivi sasa na kuamua kucheza soka na kutoa msaada mkubwa katika timu ikiwemo kutengeneza nafasi za kufunga na yeye mwenyewe kufunga mabao.

“Tumeandaa zawadi nyingine za magari mawili ambayo yapo hata kama wakitaka tuyaweke wazi hakuna shida, kikubwa tunataka tuwe na wachezaji wanaopambana kwa ajili ya timu.

“Lakini tunatarajia kupata chagamoto kubwa ya kumpata mchezaji bora anayefuata, hiyo inatokana na wachezaji wawili Ajib na Mkude kuonekana kubadilika kadiri siku zinavyokwenda na kuonyesha uwezo wa juu.

“Kama kamati tumemfuatilia kwa karibu Mkude na kuonekana kubadilika kwa kiwango kikubwa, pia Ajib ni mchezaji anayeonekana kuanza kujitambua kutokana na msaada mkubwa anaoutoa kwenye timu,” alisema Poppe.


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV