September 30, 2016


Mchakato kwenda katika mchezo wao wa kesho Jumamosi dhidi ya Simba, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, amesema imetosha kuhusiana na vita ya maneno inayoendelea kati yao na kinachofuata atawanyamazisha wapinzani kwenye mechi yao hiyo.

Pluijm ameeleza zaidi kuwa wakati mwingine haifai kuongea maneno mengi kuelekea katika mchezo huo kwa kuwa kikosi chake kinafahamu nini cha kufanya ili kunyamazisha maneno yote yanayoendelea mitaani kuanzia kwa mashabiki, wapenzi, wadau mpaka viongozi.

“Huu mchezo umewaweka wengi kwenye presha, sasa sitaki kuongea sana, kuna maneno mengi yameshaongelewa na hii ni kwa kuwa ni mchezo wenye presha kwa sababu ni moja ya utani wa jadi uliopo, sasa kwa upande wetu nadhani hatuhitaji kuongea zaidi ya kufanya kazi hiyo Jumamosi.

“Wachezaji wangu wanafahamu mashabiki wanataka nini na nini cha kufanya kuzima hii presha iliyopo kwa mashabiki na wapenzi wengi wa Yanga, kumeshakuwa na maneno mengi lakini sasa ni vizuri kukaa kimya na kufanya kitu sahihi Jumamosi hii.

“Nafahamu nakutana na Simba inayoonekana kuimarika lakini sisi tupo vizuri zaidi, tusubiri hiyo Jumamosi,” alisema Pluijm, kocha wa zamani wa Berekum Chelsea na Medeama FC za Ghana.


Yanga inayokamata nafasi ya tatu kwa pointi 10, itaingia uwanjani kuivaa Simba iliyo kileleni kwa pointi 16, kesho katika Uwanja wa Taifa, Dar ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuwabamiza Wekundu hao katika michezo miwili waliyokutana msimu uliopita. Yanga ilishinda mabao 2-0 katika kila mchezo.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic