Straika wa Yanga, Mrundi, Amiss Tambwe baada ya kutafakari kwa kina hali ya ushindani iliyopo msimu huu katika kuzifumania nyavu sasa amekuja na mbinu mpya itakayomwezesha kuibuka mfungaji bora wa ligi hiyo kwa mara nyingine tena.
Tambwe ambaye msimu uliopita alizifumania nyavu mara 21, huku msimu huu akiwa tayari ameishafunga mabao matatu anajipanga kuhakikisha anazitumia kwa asilimia 99 nafasi za kufunga ambazo atakuwa akipata uwanjani ili aweze kutimiza lengo lake hilo kwa mara ya tatu tangu alipotua hapa nchini msimu wa 2013/14 akitokea Vital’O ya Burundi.
Tambwe alisema kama asipofanya hivyo atashindwa kutimiza ndoto zake hizo kutoka na hali ya ushindani iliyopo hivi sasa ambapo kila mshambuliaji ana uchu mkubwa wa kutaka kutwaa tuzo hiyo.
Alisema mbinu hiyo ndiyo njia pekee itakayomsaidia kutimiza ndoto hiyo, hivyo kila nafasi atakayokuwa akiipata uwanjani atajitahidi kuitendea haki tofauti na hali ilivyo sasa.
“Namuomba Mungu anisaidie kwa hilo kwani natamani sana kuandika rekodi nyingine ya kuwa mfungaji bora msimu huu.
“Nataka kubadilisha gia sasa, sitaki kuona napata nafasi ya wazi na kuacha kuitumia huu ndiyo utakuwa utaratibu wangu sasa,” alisema Tambwe ambaye sasa yupo mkoani Shinyanga na kikosi cha Yanga.
0 COMMENTS:
Post a Comment