September 26, 2016

Mara baada ya Azam kupokea kichapo cha pili katika ligi mbele ya Ndanda ya Mtwara, uongozi wa timu hiyo umeibuka na kudai kwamba hakuna wa kumlaumu kutokana na kichapo hicho kwa sababu wapinzani wao waliwazidi bahati tu ambayo ndiyo iliwasaidia kupata ushindi huo.

Azam chini ya kocha wake, Mhispania, Zeben Hernandez, juzi Jumamosi ilijikuta ikiendeleza rekodi yake ya kupoteza katika Uwanja wa Nang’wanda Sijaona, Mtwara mara baada ya kuchapwa mabao 2-1 mbele ya wenyeji wao Ndanda ya mkoani humo.

Msemaji wa Azam, Jaffar Idd, alisema kwamba licha ya wao kupambana kwa ajili ya kusaka ushindi kwenye pambano hilo, bahati haikuwa ya kwao kutokana na nafasi nyingi za mabao walizozitengeneza kuishia mikono mwa kipa wa Ndanda na nyingine kuokolewa na mabeki.  

“Kiukweli hatuna wa kumlaumu kutokana na kipigo hiki cha Ndanda kwa sababu sisi tulikuwa bora zaidi ya wapinzani wetu ambao muda mwingi tulikuwa tunawashambulia lakini ndiyo hivyo, mwisho wao wameibuka vinara kwa kutufunga kibahati kwa sababu tuliwazidi kwa kila kitu.

“Bado hatuna wasiwasi wowote juu ya kufanya vizuri licha ya kwamba tumepoteza mechi mbili mpaka sasa kwa sababu kuna mechi nyingi zimebaki na kocha Zeben ameshayachukua mambo yote ambayo yamesababisha sisi kupoteza mechi hizi na ametuhakikishia kwamba tutaibuka washindi katika mchezo ujao,” alisema Idd.     


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV