Mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Yanga dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, ni kesho.
Wachezaji wa Yanga, juzi Alhamisi walipigwa na butwaa baada ya kuamshwa usiku kwa ajili ya kufanya kikao na uongozi kuweka mikakati ya ushindi.
Kitendo hicho kiliwashangaza baadhi ya wachezaji ambao walizoea kufanya kikao kama hicho nyakati za mchana au jioni.
Habari kutoka ndani ya Yanga zimesema, wachezaji waliamshwa saa 4:00 usiku na kufanya nao kikao kifupi kilichochukua kama muda wa nusu saa hivi.
“Kikao kilikuwa ni cha kawaida tu ambacho kililenga zaidi mechi yetu ya Jumapili dhidi ya Stand United, hakukuwa na jambo lolote kubwa la kutisha ila kocha alitaka kuzungumza na wachezaji muda huo kuwakumbusha majukumu yao.
“Lakini pia alitumia muda huo kuwasisitiza wachezaji kuhakikisha wanacheza kwa nguvu zao zote katika mchezo huo ili tuweze kupata ushindi ambao utawaongezea morali ya ushindi dhidi ya Simba,” alisema kiongozi huyo.
Mmoja wa wachezaji tegemeo wa Yanga ambaye hakutaka kutajwa jina, alithibitisha kufanyika kwa kikao hicho.
“Tulishangaa kuamshwa usiku ule, kwani si kawaida yetu kufanya kikao usiku lakini tuliamka na kuzungumza na kocha,” alisema mchezaji huyo. Yanga kesho inacheza na Stand mechi ya ligi kuu ikiwa nafasi ya pili na pointi 10 katika mechi nne ilizocheza huku Stand ikiwa nafasi ya nane na pointi sita.
0 COMMENTS:
Post a Comment