October 31, 2016



Na Saleh Ally
MIJADALA ya kwamba Tanzania inapaswa kupata wanasoka wengi wanaocheza nje ya Tanzania inazidi kupamba moto.

Imani kwamba wengi wakiwa wanacheza nje ya nchi, msaada unakuwa ni mkubwa katika mabadiliko na hasa katika kikosi cha timu yetu ya taifa.

Timu ya taifa inapokuwa na wachezaji wengi wanaocheza nje ya nyumbani, kunakuwa na msaada mkubwa kuliko wengi wanaocheza nyumbani.

Kuna nchi chache sana zimefanikiwa kuwa na wachezaji wanaocheza ndani lakini wakawa na timu bora ya taifa au yenye ushindani wa juu. Zaidi ni nchi tatu pekee. Misri, Sudan na Afrika Kusini na mazingira yao yanawaruhusu.

Nchi mbili, ukianza na Misri ni yenye mafanikio kitambo, matajiri lakini nidhamu ni muongozo mkuu katika maisha ya kawaida na michezo pia hasa soka, hii ni sawa na Sudan, muongozo wa kinidhamu unaendana na dini. Afrika Kusini ni kutokana na historia, wengi wameishi miaka nenda rudi bila ya kutoka nje ya nchi yao, wamepata mafanikio wakiwa ndani na wanaweza kufanya makubwa wakiwa humohumo.


Tanzania ni kama nchi nyingine za Afrika. Kwenda nje kunaweza kuwa shule bora kuliko kusoma chuo kikuu fulani. Tunaona mfano wa karibu zaidi ni Uganda ambayo wachezaji wake wengi hawachezi ligi kubwa za Ulaya lakini wamekuwa msaada mkubwa, leo wamefuzu kucheza Kombe la Mataifa Afrika.

Kote huko nimepita, nilitaka kukueleza namna ambavyo tunahitaji kuwa na wachezaji wanaocheza nje ya Tanzania. Hata kama itakuwa ni nchi za jirani au humuhumu barani Afrika, bado wanaweza kubadilika.

Ndani ya misimu miwili, Tanzania imeweka rekodi mpya ya kuwa na wachezaji wawili wanaokataa kupewa mkataba mpya na mnono kutoka katika klabu kubwa na maarufu barani Afrika, Ulaya na kwingineko duniani.

Alianza Mbwana Samatta, akakataa mkataba mnono wa TP Mazembe na kuamua kwenda KRC Genk ya Ubelgiji ambako kidogokidogo ameanza kuzoea na anafanya vizuri taratibu, Mungu atamsadia atakwenda mbali zaidi kwani mwenyewe pia ana nia.

Safari hii ni Thomas Ulimwengu, naye amemaliza mkataba wake na TP Mazembe, hataki mkataba mpya na anataka kwenda zake Ulaya. TP Mazembe bado inamhitaji, hakika hili ni jambo jema kwa Tanzania lakini mtihani mkubwa kwa wachezaji wengine.

Hakuna mchezaji hata mmoja anayecheza Ligi Kuu Bara, awe wa hapa au wale wanaotokea nje ya Tanzania, sijui Donald Ngoma, Laudit Mavugo na wengineo mwenye jeuri ya kuigomea TP Mazembe. Kila mmoja angepewa mkataba, angeuchangamkia ile mbaya, hata kama ingekuwa kutembelea meno.

Lakini Ulimwengu ambaye ni kijana mdogo tu wa Kitanzania. Anataka kusonga mbele, anataka kupiga hatua kwa kucheza Ulaya na si kubaki tena pale.

Ulimwengu tayari ameona Mazembe si saizi yake hasa wakati anataka kutimiza ndoto zake za miaka nenda rudi, hata kama wako waliomuona ni mwendawazimu.

Alionekana kama amepoteza alipoamua kurejea kutoka katika timu ya AFC ya Sweden kwenda TP Mazembe. Katokea Afrika akaenda Ulaya, akatokea Ulaya kwenda kucheza Afrika tena, sasa anarudi Ulaya akiwa na uhakika, hii ni akili kubwa.

Kujiamini kwa Ulimwengu si kumekuja tu, ni mafunzo na changamoto alizopitia akiwa TP Mazembe. Amekutana na mabeki wa kila aina, kuanzia DR Congo, Afrika, Amerika Kusini, Ulaya, Asia na kwingineko.

Sasa anataka kwenda mbele na unaona anavyojiamini.  Wengine humu ndani mko wapi, kwani Ulimwengu na Samatta ni raia wa Misri? Mmekula maharage ya wapi, vipi mmelala tu na mna visingizio tu?


Changamkeni hasa wenye umri unaowaruhusu, kwenda kupambana na changamoto nje ya Tanzania ni mapema, msisubiri kwenda kustaafu Ulaya. Amkeni.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic