October 10, 2016


LUNYAMILA


Uongozi wa Klabu ya Yanga kupitia wanachama wake, umekubali kukodisha nembo na timu yake kwa kampuni ya Yanga Yetu Ltd.

Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya mkutano wa dharura wa wanachama wa Yanga, baada ya hapo mchakato ukaanza kupitia Bodi ya Wadhamini wa Yanga ambayo Mwenyekiti wake ni Mama Karume na mwisho mkataba ukasainiwa.

Klabu ya Yanga itabaki na mali zake zote ikiwa ni pamoja na majengo, gari na mali nyinginezo. Pia itachukua fedha zote za wadhamini wa Ligi Kuu Bara ambao ni Azam Media.

Lakini timu ambayo ni gharama kubwa, itakuwa chini ya Yanga Yetu pia nembo ambayo kampuni hiyo imesema itapambana kuifanya ianze kuingiza faida.

Hasara ikipatikana, itabaki kuwa ya Yanga Yetu Ltd na kama kutakuwa na faida klabu itachukua asilimia 25 na kampuni hiyo asilimia 75.

Wakati Wanayanga walikubaliana na hilo, BMT imeibuka na kuandika barua iliyojikanganya na kuzua maswali mengi. Barua hiyo inaeleza kufuatwa kwa taratibu jambo ambalo tayari limeufanya uongozi wa Yanga kuitisha mkutano mwingine wa dharura Oktoba 23.

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Edibily Jonas Lunyamila, ameeleza kusikitishwa na BMT na kusema inawachanganya Wanayanga.

“Si sahihi BMT kusema utaratibu haukufuatwa, si sahihi kusema eti suala hilo linaweza kusababisha vurugu wakati wao ndiyo wanaotaka kusababisha.

“Wanayanga kwenye kikao tulikubaliana kwa pamoja, mchakato ukaanza na umechukua zaidi ya miezi miwili. BMT walikuwa wapi, wanataka nini sasa hivi? Wasiwachanganye Yanga.

“Wanachama ndiyo wenye mali, kuna wajumbe wa bodi ya wadhamini. Sidhani kama kuna mtu anataka Yanga ipotee.
“Najua mabadiliko haya yanawaumiza wengine, utaona hata kwenye tiketi za elektroniki wako ambao hawataki kwa kuwa maslahi yao yameguswa. Mfano Mzee Akilimali, anaonekana kaguswa, hawezi kukubali mambo hivihivi.

“BMT wanapaswa kuonyesha wanalenga kuisaidia Yanga, si mwekezaji amepatikana wanataka wamtibue na kutuvuruga. Walikuwepo tokea mwanzo, hawakusema kitu, vipi wanaibuka leo? Maana yake sisi sote hatujui lolote, nahisi kuna kitu nje ya hili. Nawasihi waiache Yanga ifanye mambo yake,” anasema Lunyamila.

Ukiachana na Lunyamila, wadau wengine wa Yanga nao walipata nafasi ya kutoa maoni.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic