October 26, 2016


Kocha Juma Mwambusi ndiye ataiongoza Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu JKT kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, leo.

Mwambusi tayari amesema, hana mpango wa kuhamia Prisons na wala hajajiuzulu Yanga kama ambavyo imeelezwa.

Akili yake anaielekeza katika mechi ya leo na lengo kubwa ni kuhakikisha wanafanya vizuri katika mechi hiyo.

Yanga inaivaa JKT ikiwa bila ya kocha wake, Hans van der Pluijm ambaye amebwaga manyanga baada ya George Lwandamina kutoka Zambia kufika nchini na kuzungumza na Yanga.

Aidha, Kocha wa JKT Ruvu, Malale Hamsini, ameibuka na kuwatambia wapinzani wao Yanga kwa kusema kuwa wasifikiri watapata mteremko katika mchezo wa leo.

Yanga leo inavaana na JKT Ruvu kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar, ikiwa imetoka kuwachapa Kagera Sugar mabao 6-2.

Kocha Mkuu wa JKT Ruvu, Malale Hamsini, amesema kuwa, siyo mara ya kwanza kukutana na Yanga, hivyo wasifikirie watapata mteremko kutokana na kuwafunga Kagera Sugar mabao 6.

“Kikosi chetu kipo vizuri na timu ipo kambini, hakuna majeruhi hata mmoja zaidi ya Michael Aidani aliyekuwa majeruhi wa muda mrefu lakini kwa sasa ameshaanza mazoezi.

“Lakini Yanga wasitegemee mteremko kwa kupata matokeo mazuri kwetu kutokana na kuifunga Kagera Sugar mabao sita kwani tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mechi hiyo.

“Siyo mara yetu ya kwanza kukutana na Yanga, hivyo tunaiona ni timu ya kawaida na kikosi chetu kipo vizuri kwa ajili ya kupambana nao,” alisema Malale.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV