October 10, 2016


Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, amemtahadharisha kiungo wake mshambuliaji, Shiza Kichuya, akimwambia hatakiwi kubweteka na sifa anazoendelea kuzipata na badala yake aongeze bidii ndani ya uwanja.

Kichuya ambaye ni mchezaji tegemeo kwenye timu hiyo, ameshaifungia Simba mabao matano na ndiye anayeongoza kwenye chati ya ufungaji kwenye Ligi Kuu Bara huku akikumbukwa kwa kuipa timu yake pointi tatu dhidi ya Azam FC na pointi moja kwa bao maridadi la dakika ya 87 dhidi ya Yanga.

OMOG
Kiungo huyo mwenye kasi kubwa ndani ya uwanja, alijiunga na Simba msimu huu wa Ligi Kuu Bara akitokea Mtibwa Sugar kwa dau la Sh milioni 30.

Omog alisema hampangi mchezaji katika kikosi chake kutokana na umaarufu huku akitaja juhudi binafsi ndani ya uwanja na kujituma kuwa ndiyo kigezo anachokitumia katika kupanga timu.

Omog alisema, anafurahishwa na kiwango kikubwa kinachoonyeshwa na Kichuya uwanjani ambacho kimemfanya kuonekana bora na tegemeo kwenye timu kubwa kama Simba.

Aliongeza kuwa, kikubwa anachotakiwa kufanya kiungo huyo, ni kuendelea kulinda kiwango chake ili kisishuke kwa kutimiza majukumu yote atakayopewa katika timu.

"Wachezaji wengi wanafeli katika kupata mafanikio kutokana na kuridhika, pia kubweteka baada ya kulewa sifa pale wanapofanya kitu kizuri na kusifiwa.

"Hali hiyo, sitaki imtokee Kichuya baada ya kuifungia timu yake bao la kusawazisha katika dakika ya 87 kwenye 'derby' na Yanga iliyochezwa hivi karibuni.

"Kikubwa anachotakiwa kufanya hivi sasa ni kuendelea kulinda kiwango chake ili kisishuke kwa kutimiza majukumu yote atakayopewa katika timu ikiwemo kufunga na kutengeneza nafasi za kufunga mabao," alisema Omog.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV