Unaweza ukasema hii kali, maana benchi la ufundi la Simba linaloongozwa na Mcameroon, Joseph Omog na Mganda, Jackson Mayanja, limeonyesha nia ya dhati ya kutwaa ubingwa kwa msimu huu ambapo sasa limetangaza hali ya hatari kwa wachezaji ambao wanacheza kwa ajili ya kuwafurahisha mashabiki ‘shoo’ kwa kuwapiga kanzu au matobo wapinzani wao kuwa benchi litawahusu.
Simba imekaa miaka minne bila ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu tangu mwaka 2012 ambapo kwa sasa kikosi hicho kina nafasi kubwa ya kuutwaa ubingwa huo kutokana na kuwa kileleni mwa ligi baada ya mechi 14, kikiwa na pointi 35, tano mbele ya Yanga iliyopo nafasi ya pili.
Mayanja ameweka wazi kuwa wameamua kuchukua maamuzi hayo kwa sababu wanataka kuwafanya wachezaji wote wawaze kuhusiana na kupata matokeo zaidi na kuachana na mpira wa kiburudani ambao hauna maana yoyote kwenye kipindi hiki kwa upande wao.
“Tumewapiga marufuku wachezaji kucheza mpira ambao hautakuwa na maana kwa upande wetu yaani sasa hakuna matobo, kanzu wala chenga ambazo hazina maana na badala yake tumewaambia wawe wanawaza kupata ushindi na pointi tatu.
“Na kama tukiona mchezaji anafanya hivyo, sisi benchi la ufundi tunamtoa na kumpa mtu mwingine nafasi yake na hataweza kucheza mpaka pale atakaporekebisha makosa yake kwa sababu tumepania kutwaa ubingwa hivyo kuwa na mtu wa namna hiyo kunaweza kusababisha tukakosa ushindi pale utakapohitajika,” alisema Mayanja.
0 COMMENTS:
Post a Comment