November 9, 2016


Na Saleh Ally
VINARA wa Ligi Kuu Bara, Simba wana pointi 35 baada ya kucheza mechi 14 za ligi hiyo wakiwa wameshinda 11.
Simba walicheza hadi kufikia mechi 13 bila ya kupoteza hata moja. Kati ya hizo ushindi ni mechi 11, na sare mbili. Kila Mwanasimba alikuwa anazungumza lugha inayofanana, mafanikio.

Kila Mwanasimba alikuwa akiamini kwamba inawezekana kabisa Simba itacheza na kumaliza msimu bila ya kufungwa hata mechi moja.

Hii ilitokana na mambo mawili, kwanza ni mwendo wa kikosi cha Simba ambacho hakuna mechi kilishinda bila ya kuonyesha soka safi linalopangika kuanzia mwanzo yaani upande wa zone ya Simba hadi upande wa pili wa  timu pinzani.

Pili ni Kocha Joseph Omog ambaye ndiye pekee aliyewahi kuiwezesha Azam FC kubeba ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya kwanza na ya mwisho, tena ikiwa haijapoteza hata mechi moja.

Hivyo Wanasimba wakawa wanaamini kabisa, Simba inaweza kufikia mwishoni mwa mzuguko wa kwanza kwa kucheza mechi 15 bila kupoteza, halafu ikaanza mzunguko wa pili wa mechi nyingine 15 bila ya kupoteza pia.

Baada ya Simba kukutana na kisiki katika mechi yake ya 14 kwa kutwangwa na African Lyon kwa bao 1-0, hapo ndiyo unaweza kushangazwa na Wanasimba eti wamechanganyikiwa kuona timu hiyo imepoteza mechi.
Wamechanganyikiwa hasa, kila mmoja anasema lake ingawa kila kinachosemwa unaweza kukijumlisha kwa neno moja tu la kihafidhina, lawama.

Naliita neno hili ni la kihafidhina kwa kuwa tafsiri ya uhafidhina ni watu wasiotaka mabadiliko hasa yanayohusiana na uingizwaji wa mambo mapya. Katika michezo, lawama ni sawa na uhafidhina kwa kuwa umekuwa ukipinga kila kilicho wazi ilimradi kila mmoja hakubali tu kitu fulani.

Ndiyo unapoona unashangazwa sana au kuchekeshwa kuona eti kuna mashabiki wa timu fulani wamechanganyikiwa sana baada ya timu yao kupoteza mechi moja baada ya kucheza mechi 13 bila ya kupoteza hata moja.

Timu iliyoshinda mechi 11, iko kileleni mwa ligi, inapaswa vipi kujichanganya kwa kupoteza mechi ambayo wazi ilionekana kuwa wao ndiyo walicheza vizuri lakini mwisho wakaadhibiwa kutokana na makosa yao.

Katika soka, ukifanya kosa unaadhibiwa, huu ni utaratibu wa kawaida kabisa. Simba walipanda wote wakawa wanashambulia tu. Kwa kuwa African Lyon tokea kipindi cha kwanza waliamua kubaki nyuma na kufanya mashambulizi ya kushtukiza wakionyesha wazi walitaka sare, Simba wakajisahau, ‘ukuta ukawaangukia’.

Wale mashabiki wa Simba waliochanganyikiwa na kuanza kulaumu wachezaji wamewaangusha, wachezaji hawakuwa vizuri, wachezaji walikuwa tatizo, kocha Joseph Omog na msaidizi wake, Jackson Mayanja hawakuwa na mpango mbadala au plan B, walijiuliza Simba ilishindaje mechi 11?
Wengi waliolaumu ni wale wasiojua sahihi mpira unapitia wapi, njia zake zipi. Kwa kuwa tabia ni ya kihafidhina ya kutaka kupinga kila kitu hata kwenye hali halisi. 

Walishindwa hata kukumbuka nyuma kwenye mazuri kwa asilimia 90, wakaizungumzia asilimia 10 mbaya kwa mapana kabisa. Hii si sawa hata kidogo.

Mashabiki wanaolalamika, kipi kinawafanya walalamike hivyo wakati misimu miwili mitatu, Simba ilikuwa inapoteza rundo la mechi na mwisho walipigiana makofi na kupeana moyo wafanye vema mechi zinazofuata na ikawa hivyo.

Simba hii ndiyo imeanza kuimarika, kocha huyu ndiyo msimu wake wa kwanza akiwa ameing’oa kwenye tope. Huenda kufungwa kwa Simba kutakuwa faida kubwa katika mechi yao dhidi ya Prisons pia kwa mzuguko wa pili.

Huenda hata wachezaji wa Simba walifikiri wao hawafungiki kutokana na walivyoaminishwa na mashabiki, hili ni jambo baya kabisa katika soka kokote kule.

Timu bora, zenye makocha bora na wachezaji mahiri zinafungwa mara kwa mara. Tena zenye kila mpangilio bora wa kila kitu. Hii inaonyesha katika soka suala “kupoteza” si geni na litaendelea kuwepo kila kukicha na ndiyo maana ya kutengeneza umakini, kujituma na kuweka malengo.
Acheni kulalama bila sababu za msingi, acheni kuamini kuzungumza sana mbele ya watu ukionekana unalaumu sana ndiyo kujua sana au kuonyesha ujanja wa ujuvi wa mambo.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic