November 21, 2016Na Saleh Ally
KAMA utakuwa na kumbukumbu vizuri, mshambuliaji Emmanuel Okwi hajawahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara. 

Msimu wa 2013-14, aliifungia Yanga mabao mawili tu, msimu uliofuata wa 2014-15 akiwa na Simba ambao ni msimu wake wa mwisho akafunga mabao 10.

Okwi, raia wa Uganda, hajawahi kuwa mwanasoka bora wa ligi hiyo na hajawahi kuwa na mafanikio makubwa ambayo yanaweza kuwalazimisha Simba kufunga kila kitu na leo wakamuwaza yeye tu!

Simba ndiyo wanaomtamani Okwi, wanaomuwaza na kumzungumzia wakati yeye akiendelea na mambo yake katika Klabu ya SonderjyskE ya nchini Denmark ambako ameshindwa kuonyesha cheche tangu ametua huko na kujiunga nao akitokea Simba.

Okwi amekuwa biashara nzuri kwa Simba, mwaka 2013 ilimuuza kwa dola 300,000 (zaidi ya Sh milioni 600) kwenda Etoile du Sahel ya Tunisia, uongozi wa wakati huo ukafanya ‘blanda’ kwa kutolipwa hadi zilipokuja kulipwa kwa amri ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa). Kwa hesabu za kibiashara, Simba ilipata hasara kubwa kwa kuwa fedha hizo zilibaki muda mrefu mikononi mwa wanunuzi ambao ni Etoile du Sahel.

Okwi, alishindwa kufanya vema Etoile, akarejea nchini na kujiunga na Yanga, nako akashindwa kufanya vema tena hadi alipojiunga na Simba ambayo unaweza kusema hakufanya vizuri tena ila alijitahidi. Maana hakuipa Simba ubingwa zaidi ya ahueni, akaondoka tena kwenda Denmark.

Okwi ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa uwanjani lakini mwenye matatizo mengi na uongozi wa Simba unalijua hili. Amekuwa akiwasumbua mara nyingi na wanalalamika.

Mara kadhaa, wameeleza kutoridhishwa na mambo kadhaa waliyoyaita ni utovu wa nidhamu. Yanga pia walilalamika hivyo na mwisho wakaingia katika mgogoro mkubwa. 

Wako viongozi wa Simba ambao wamekuwa wakieleza namna ambavyo wamekuwa wakimhimiza Okwi kwa zawadi kwamba ahakikishe anawamaliza Yanga au timu fulani na kweli atafanya hivyo.

Inaonekana kote alipokwenda, hakuna mambo ya zawadi na mambo yanakwenda kwa kufuata weledi, huenda limekuwa jambo ambalo limechangia naye kushindwa kufanya vema zaidi.

Yuko Denmark na mambo hayaendi vema kama ambavyo alivyokuwa Tunisia. Lakini hata alipokuwa Yanga, pia mambo hayakwenda vizuri. Wanaomjulia ni Simba pekee, huenda wanajua zaidi kubembeleza.

Simba imekuwa ni timu yenye wachezaji wengi wakubwa ambao waliwahi kupita. Kwa wanaowakumbuka akina William Fanbullah kutoka Liberia, Mark Sirengo wa Kenya na wengine, walikuwa watu kweli na hawakuhitaji zawadi au bakhshishi ili kufanya vema zaidi.

Leo hawapo ndiyo maana Simba ilimpata Okwi akafanya vizuri. Kumbuka vizuri hata yeye mwanzoni pia hakuweza kung’ara, karibu msimu mzima alikuwa ndiyo kama mtu anayeamka.

Baadaye alianza kufanya vizuri na kuwa gumzo. Lakini sasa ni wakati wa Simba kujijenga upya na kuachana na kuwa tegemezi kwa Okwi ambaye umri unakwenda na pia bado kwao anaweza kuwa bora na wakati mwingine mzigo mzito.

Okwi anaweza kurejea Simba akasaidia kurejesha morali, lakini anaweza kurudi akaiua vilevile. Simba haipaswi kuwa tegemezi kwa mchezaji mmoja kiasi hicho hadi kufikia kuwaza akiondoka, basi haiwezi kuinuka hata hatua moja mbele.

Katika mechi 15 za mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, Simba imeshinda mechi 11, sare mbili na imepoteza mbili. Bado iko kwenye kiwango bora bila ya Okwi. Inaweza kwenda mbele bila ya yeye kama itakuwa na mawazo chanya.

Nimesikia viongozi wakisema hawana taarifa na suala hilo. Lakini wako wanaoamini lipo, mashabiki ndiyo usiseme. Lakini ningekuwa nimepewa nafasi ya kutoa ushauri katika hili, ningewashauri Simba kuachana na Okwi naye aendelee na maisha yake. Lazima wawaze kamili, kuwa baada ya Okwi ni nini na kipi sahihi. Si kila akiondoka wao hawana namna, huu ni upungufu wa kujiamini!

Wako wanaoweza kuwa bora ndani ya Simba, wanahitaji muda na Simba haipaswi kuwa na papara na kufanya vitu kwa maneno ya mashabiki, badala yake ingalie mipango thabiti iliyo katika njia sahihi.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV