November 21, 2016Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime, amewataka viongozi wa Azam FC wampatie mshambuliaji wa timu hiyo anayeitumikia Simba kwa mkopo, Ame Ally ‘Zungu’ ili aiongezee nguvu safu yake ya ushambuliaji ambayo amedai kuwa haipo sawa kama anavyotaka iwe.

Maxime amefikia hatua hiyo baada ya kuona benchi la ufundi la Simba halimtumii mchezaji huyo tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Azam ambapo mpaka sasa amefanikiwa kucheza mechi nne tu kati ya 15 na zote amekuwa akitokea benchi.

Maxime amesema kuwa anawashangaa Simba kwa nini hawampatii nafasi mchezaji huyo wakati anaamini kuwa ana uwezo mkubwa wa kuzifumania nyavu kushinda baadhi ya wachezaji klabuni hapo.

Alisema kama wanaona hafai, basi wampatie yeye halafu waone ni jinsi gani atakavyokuwa anazifumania nyavu kama ilivyokuwa zamani wakati alipokuwa naye Mtibwa Sugar.

“Nipo katika harakati za kutafuta washambuliaji na hivi sasa nafanya mazungumzo na baadhi yao kutoka timu mbalimbali za ligi kuu.

“Hata hivyo, kuhusiana na Ame Ally hakika sijui kwa nini Simba hawamtumii, kama vipi Azam ambao ndiyo wanaommiliki wanipatie  mimi waone jinsi gani atakavyokuwa akiifanya kazi yake ya kufunga kama wakati ule nilipokuwa naye Mtibwa Sugar,” alisema Maxime.

Kagera Sugar, licha ya kuwa katika nafasi ya nne, imefunga mabao 16 tu katika michezo 15 ya mzunguko wa kwanza huku pia ikiwa imefungwa mabao 16.

SOURCE: CHAMPIONI

1 COMMENTS:

  1. Maxine mbn yes kashindwa kumtumia Themi Felex wakati Mbeya City alikuwa anafunga, aanze kumtumia huyo kwanza

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV