Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’, juzi usiku alikamatwa na askari wa Kitengo cha Kupambana na Kuzuia Madawa ya Kulevya kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wa jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo la kukamatwa lilitokea siku chache tangu bondia mwingine Mtanzania, Thomas Mashali alipofariki dunia kwa kushambuliwa na watu wasiojulikana maeneo ya Kimara jijini Dar.
Dullah alikamatwa wakati anaelekea nchini Ujerumani kwa ajili ya kwenda kupambana na bondia, Toni Kraft kwenye Ukumbi wa Ballhaus Forum uliopo Jiji la la Munich.
Bondia huyo alikamatwa ikiwa ni muda mchache tangu atoke kwenye maziko ya Mashali, juzi mchana Makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Dullah amesema alikamatwa na askari hao saa 5:00 usiku uwanjani hapo na kutolewa jana Alhamisi saa saba mchana baada ya kuhojiwa.
Dullah alisema mara baada ya kukamatwa, askari hao walimsachi na kugundulika hakuwa na kitu chochote kibaya alichokuwa amekibeba ikiwemo dawa za kulevya ambazo walikuwa wakihisi amebeba kuzipeleka Ujerumani.
Alisema kuwa, safari yake hiyo juzi usiku ilishindikana, badala yake leo (jana) saa tano usiku ataondoka kuelekea Ujerumani kwa ajili ya pambano hilo linalotarajiwa kufanyika kesho Jumamosi.
"Hadi inafikia hatua hii ya mimi kukwamishwa kwenda kupigana Ujerumani, keshokutwa (kesho) Jumamosi, mimi tayari nimeshamjua mbaya wangu, subirieni nirudi halafu nitamtaja.
"Ishu ilikuwa hivi, mimi nilifika uwanja wa ndege saa tano usiku Jumatano kwa ajili ya kuanza safari ya kwenda Ujerumani, ghafla nikiwa kwenye ukaguzi, askari walinikamata wakinituhumu nimebeba dawa za kulevya, kitu ambacho siyo sahihi.
"Kiukweli kabisa, mabosi wangu walinisaidia uwanja wa ndege hapo na kutoka leo (jana) saa saba mchana baada ya kunifanyia uchunguzi na kunihoji, lakini nashukuru hawajanikuta na kitu chochote na leo Alhamisi (jana) usiku ninatarajia kuondoka,” alisema Mbabe.
0 COMMENTS:
Post a Comment