November 28, 2016


Kocha mpya wa Mwadui FC, Ally Bushir ‘Benitez’, ameweka bayana mipango yake ndani ya timu hiyo, huku kubwa akisema anataka kuijenga kuwa Mwadui mpya itakayosumbua mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.

Bushiri ambaye juzi alipewa mkataba wa mwaka mmoja na nusu wa kuinoa Mwadui, anachukua mikoba ya Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye aliachana na timu hiyo Oktoba, mwaka huu.

Bushiri ambaye alikuwa kocha wa KMKM ya Zanzibar, alisema: “Tayari nimejiunga na Mwadui na hapa tunavyoongea nipo Shinyanga katika Mji wa Mwadui na kesho (leo Jumatatu) Mungu akipenda nitaanza kazi ya kuinoa hii timu kwa ajili ya mzunguko wa pili.

“Nimepewa mkataba wa mwaka mmoja na nusu ambao utamalizika msimu ujao. Nimekuja hapa nikiwa na malengo makuu mawili, kwanza kuitoa timu katika nafasi mbaya iliyopo na kumaliza nafasi nne za juu.

“Tayari nimepewa DVD nane za mechi za mzunguko wa kwanza, nimeona vijana wapo safi lakini kuna upungufu mdogo ambao naahidi nitaufanyia kazi katika kuijenga Mwadui mpya ambayo mzunguko wa pili wa ligi itakuja kuwa tishio.”

Mwadui ambayo huu ni msimu wake wa pili katika Ligi Kuu Bara, imemaliza mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo ikiwa nafasi ya pili kutoka chini ikijikusanyia pointi 13 baada ya kucheza mechi 15.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV