November 21, 2016

PETER MANYIKA AKIWA NA MPENZI WAKE

Baada ya safari ndefu, hatimaye kipa wa Simba, Peter Manyika, amemuangukia baba yake mzazi, Manyika Peter kwa kumuomba msamaha kutokana na vitendo vyake vya utovu wa nidhamu alivyokuwa akifanya, vilivyosababisha aporomoke kiwango.

Awali, msimu uliopita kipa huyo aliingia katika mgogoro na mashabiki wa timu hiyo kufuatia kuweka picha ya aliyekuwa akidaiwa ni mpenzi wake katika Mtandao wa Kijamii wa Instagram na kisha kuwatukana mashabiki hao kwa kuandika: “Anayesema huyu ananishusha kiwango aje adake yeye.”

MANYIKA PETER

Kufuatia kauli hiyo, Manyika alianza kupoteza nafasi ya kucheza katika kikosi cha timu hiyo licha ya baba yake mzazi kufanya jitihada za kumkanya ambapo msimu huu chini ya kocha Mcameroon Joseph Omog hajafanikiwa kucheza mchezo wowote wa Ligi Kuu Bara huku kiwango chake kikidaiwa kuporomoka zaidi.

Manyika ambaye baba mzazi wa mchezaji huyo, alisema kuwa mtoto wake ameamua kumuomba msamaha kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu alivyokuwa akifanya hapo awali hali iliyomlazimu kuanza kumtengeneza upya ili arejee kwenye kiwango chake cha awali. 

PETER MANYIKA

“Kijana wangu amerejea katika kituo chetu cha TGC kwa ajili ya kujiandaa upya lakini kwanza aliomba msamaha akiwa na baadhi ya wakubwa walimsaidia kumuombea na uzuri wake mwenyewe amekiri kosa.

 “Unajua kituo kinafundisha misingi mizuri  kwa makipa wetu kwa sababu hii ndiyo kazi yao, sasa yeye kuna wakati aliona anaweza kujisimamia mwenyewe lakini matokeo yake akawa ameanguka zaidi badala ya kupanda, nadhani sasa ameona ni wakati mwafaka  wa kurejea kuomba msamaha ili aweze kujiweka sawa,” alisema Manyika.

Manyika mkubwa aliwahi kuidakia Yanga kwa mafanikio makubwa, pia ni kati ya makipa waliodaka muda mwingi katika kikosi cha Kilimanjaro Stars na Taifa Stars.


Kipa Juma Kaseja ndiye alimaliza zama za kutamba za Manyika, yeye akiwa anachipukia kutokea Moro United na baadaye kujiunga na Simba.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV