November 24, 2016
Na Saleh Ally
UNAPOZUNGUMZIA mchezo wa ngumi hapa nyumbani, basi lazima uanze na Rashid Matumla. Huyu alipewa majina ya Snake Boy na Snake Man baadaye.

Bondia Mtanzania aliyeanza kuonyesha cheche za kuwagaragaza mabondia nyota wakiwemo wazungu na kubeba ubingwa wa dunia kama ule wa IBO, UBU na kadhalika.

Alibeba hadi mataji matano ya dunia akiwa katika kiwango chake bora mwanzoni mwa miaka ya 2000, kabla ya kuanza kuporomoka. 

Sasa Matumla ni mwananchi wa kawaida, si mwenye fedha angalau za kuweza hata kujinunulia usajifiri. Anaishi maisha ya kawaida au ya chini na mwenye anakubali, kuwa mabondia wengi mwisho wao ni tabu.

Wakati mwingine, Matumla aliamua kuwa mlinzi au mtuliza fujo katika moja ya ukumbi maarufu wa burudani jijini Dar es Salaam. Lakini sasa ametulia nyumbani, zaidi akitegemea juhudi za mkewe ambaye anafanya biashara ndogondogo kuendelea kuonyesha maisha yao.SALEHJEMBE ni blog inayopenda kufanya mambo kwa uhakika, lilifunga safari hadi nyumbani kwa Matumla. Bingwa huyo wa zamani wa dunia, anaishi katika eneo la bondeni kabisa, sehemu inajulikana kama Keko Magurumbasi.

Matumla ni mtu mstaarabu sana, mkimya na asiyependa makuu. Alianza kwa kuwakaribisha Championi nyumbani kwake na baada ya hapo akawa muwazi kwa kila swali. Lakini ndoto yake kubwa ni kuendeleza vijana, jambo ambalo pia amefeli.


SALEHJEMBE: Vijana unataka kuwaendeleza lakini unasema huna uwezo, unaweza kuelezea?
Matumla: Ni kweli, nakumbuka gazeti lenu liliwahi kunisaidia nikaanzisha kituo cha kulea watoto kimichezo, pia wadau wengine walijitokeza. Lakini sasa vifaa vimechakaa, inakuwa kazi ngumu. Hivyo watu wajitokeze wanisaidie, nami huu ujuzi niwaachie wengine.

SALEHJEMBE: Ulifanikiwa hata kidogo ulipoanza kufunza watoto na vijana?
Matumla: Wako mabondia bora kabisa, watoto wanaupenda huu mchezo. Tatizo kubwa inakuwa mwendelezo. Hauwezi kuwa bondia bora bila ya kupata mafunzo sahihi ya kutosha. Pia unatakiwa kupata mwendelezo wa mechi nyingi zaidi kama ilivyokuwa mimi.

SALEHJEMBE: Unafikiri bondia asipopata mechi za kutosha ni tatizo. Mimi nilifikiri akicheza mfululizo anachoka?
Matumla: Hapana, kuna mechi za mazoezi na mechi za mashindano. Hata mashindano yenyewe yanategemea ni kiwango kipi? Lakini mimi nilianzia chini, nikaendelea na ndiyo maana baadaye nikawa bora kabisa. Bondia anapaswa ajifunze mengi katika kila mechi. Hata ukali wa ngumi, anapaswa ajifunze unakuwaje, yaani anapopigwa, anasikiliziaje maumivu. 


SALEHJEMBE: Uliwahi kusema unashauri mashindano ya vijana, labda yafanyike kwa utaratibu upi?
Matumla: Vizuri kuwa na mashindano ya vijana. Si unaona mchezo wa soka, kila siku watu wanalia na vijana. Lakini ngumi watu wanataka wacheze wakishakuwa watu wazi, hii haiwezi kuwa sahihi. Hauwezi kupata mabondia bora.


SALEHJEMBE: Sasa unaendelea na kunoa vijana au umeacha?
Matumla: Ninaendelea, kuna jamaa pale Mtoni, Temeke amejitolea na kutupa nafasi. Lakini kama nilivyokueleza mwanzo, tatizo letu kubwa limekuwa ni vifaa.


SALEHJEMBE: Kama binadamu wa kawaida, unategemea nini kuendesha maisha yako?
Matumla: Kweli najisikia vibaya sana, hata kujibu swali hili lakini naweza kusema niponipo tu.


SALEHJEMBE: Upoupo Rashid, kivipi labda?
Matumla: Nipo nyumbani, zaidi ni hiyo kwenda kuwafundisha hao vijana kidogo. Lakini naweza kusema sasa namtegemea mke wangu ambaye ana biashara yake ya kuuza nguo. 


SALEHJEMBE: Anauza nguo zipi, wapi?
Matumla: Kweli anajitahidi sana, anauza nguo Keko juu kule. Unajua kuna wakati nililala ndani muda mrefu sana, ilikuwa ni kutokana na kuugua mgongo. Unajua kutokana na mazoezi makali kwa muda mrefu, mabondia husumbuliwa sana na mgongo.

SALEHJEMBE: Sasa unaendeleaje na mgongo?
Matumla: Kwa kweli ninaweza kusema naendelea vizuri na niko gado hasa, ninashukuru.SALEHJEMBE: Mabondia wengi hupata matatizo ya kichwa kutokana na msumbwi mfululizo tena kwa miaka mingi, wewe vipi?
Matumla: Namshukuru Mungu kwa kweli, unajua nilikuwa mzuri wa kukwepa ndiyo maana wakanipa jina la Snake Boy. Sikupenda kuguswa kichwani na hiyo imenisaidia


SALEHJEMBE: Unauonaje mchezo wa ngumi unavyokwenda kwa kipindi hiki?
Matumla: Wako vijana wanajitahidi ingawa naona juhudi na nidhamu ya mchezo inapotea kabisa. 


SALEHJEMBE: Labda inapotea kivipi?
Matumla: Vijana wanachipukia, wakifanya vizuri kidogo basi wanaona hakuna tena kama wao na wanakuwa wajeuri.

SALEHJEMBE: Unaweza kumtolea mfano mmoja wao?
Matumla: Mfano mzuri kuna huyu Dulla Mbabe, anakuja vizuri kabisa. Niliona anapigana, ni bondia mzuri na ana nguvu. Tatizo lake anatumia zaidi nguvu tu, akichanganya na akili, atakuwa hatari sana. Lakini akiendelea hivyo hatatamba muda mrefu.


SALEHJEMBE: Sasa hiyo ndiyo nidhamu ulikuwa unaizungumzia?
Matumla: Nidhamu mfano wake uko hivi; nimesikia Dulla kaambiwa akapigane na Cheka, kuna watu wameniambia amegoma. Anadai Cheka atakuwa kwao na watu hawaingia wengi. Kama nilichoambiwa ni kweli, hii si sawa hata kidogo. Bondia haangalii suala la watu wala anapigania mkoa gani, anaangalia maslahi yake na kama ni watu, popote ukipigana vizuri watakuja tu na kukushangilia. Mbona mimi nilimfuata Cheka Morogoro na nilikuwa bondia mkubwa?


SALEHJEMBE: Pamoja na kutwaa ubingwa wa dunia, maisha yanaonekana ni magumu sana, leo unaishi bondeni, pia nilipata taarifa wewe uliamua kuwa mlinzi wa getini kwenye ukumbi ili kuendesha maisha, hili unaliezea vipi?
Matumla: Dah!

TAFADHARI fuatilia KESHO sehemu ya pili na ya mwisho ya mahojiano haya na Rashid Matumla anayeaminika kuwa bondia bora kabisa kuwahi kutokea nchini hasa katika ngumi za kulipwa hasa kwa waliofanya kazi hapa nyumbani.


KESHO ataelezea kuhusiana na suala lake la kuwa mlinzi wa getini, suala la Jamal Malinzi ambaye alimtoa jeshini na kadhalika.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV