November 25, 2016Siku chache baada ya uongozi wa Mwadui FC kuweka bayana kumhitaji Kocha Msaidizi wa Simba, Mganda, Jackson Mayanja ‘Mia Mia’ ili kurithi mikoba ya Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, nyota imezidi kumuwakia Mganda huyo baada ya kutakiwa na timu ya taifa ya Somalia.

Mia Mia ambaye yupo nchini kwao kwa mapumziko kabla ya kurejea Bongo ndani ya siku tatu hizi, amekutana na maofisa wa shirikisho la nchi hiyo lakini akachomoa dili hilo kwa kile alichosema bado ana mipango endelevu na Simba.

Akizungumza kutoka Uganda, kiungo huyo wa zamani wa Esperance ya Tunisia, alifunguka kuwa licha ya kuwasikiliza lakini siyo rahisi kuondoka Simba inayofanya vema kwa sasa na kwamba malengo yao na mkuu wake (Joseph Omog) ni kuhakikisha wanaipa ubingwa.

“Bahati mbaya sana nina mkataba wa miaka miwili Simba. Kweli maofisa wao walinipigia simu na kunieleza nia yao (kuwa kocha wa timu ya taifa), sijawapa jibu.

“Hata kama ofa yao ni nzuri, lakini jambo la kuzingatia ni wapi ulipo. Simba inafanya vizuri kwa sasa na hii yote ni matunda yetu kama benchi la ufundi. Mikakati yetu ni kuhakikisha tunachukua ubingwa, kwa hiyo hata kama sijawapa jibu la mwisho lakini sidhani kama nitashawishika kihivyo.

“Najua wapi tumeitoa Simba mpaka leo inaonekana inafanya vizuri zaidi. Ndiyo maana hata Mwadui waliponitafuta sikutaka kuwazia nafasi hiyo hata kama wangeniambia kiasi kizuri cha fedha,” alisema.

Wakati huohuo, Mayanja amesema: “Tulimaliza vibaya mzunguko wa kwanza, hivyo tunatakiwa kujipanga vilivyo katika mzunguko wa pili kwa kuwa na umoja wa hali ya juu kwa sababu hali inavyoonekana hautakuwa mchezomchezo.


“Mashabiki wetu nao waendelee kutuunga mkono kama ilivyokuwa mzunguko wa kwanza, wasife moyo kwa matokeo tuliyoyapata dakika za mwisho, wakifanya hivyo tunaweza kutimiza mikakati yetu.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV