KIGANJA |
Na Saleh Ally
KAKA wa bondia Thomas Mashali alikuwa akilalamika kuhusiana na namna serikali ilivyoshindwa kuonyesha ushirikiano wakati wa msiba wa ndugu yake.
John Zunda unaweza kumuita binamu wa marehemu wa Mashali kwa kuwa hawa wamezaliwa na ndugu, yaani baba mkubwa na baba mdogo. Hakufurahishwa na serikali kuonekana kuwatenga wakati wa msiba huo.
Alifikia hatua ya kuwaza vibaya, kwamba labda kwa kuwa kuna taarifa za kukanganya kuhusiana na kifo cha Mashali zikiwemo zinazomhusisha na wizi au vurugu, ndiyo maana serikali imeamua kukaa kando katika suala hilo la msiba.
Najua Zunda alikuwa na majonzi, hakufurahishwa na hali hiyo kama mfiwa yeyote na anaweza kufikiria lolote.
Waombolezaji nao wakati wakiushusha mwili wa Mashali kaburini ikiwa ndiyo safari yake ya mwisho kabisa duniani, waliamua kuimba wimbo wa taifa wakionyesha kiasi gani wanaamini alilitumikia taifa na aliliwakilisha wakati mwingine kama mwanamichezo.
Siamini kama serikali inaweza kumtenga mtu kama Mashali kwa sababu ya hisia bila ya kuwa na ukweli. Lakini kilichotokea kilikuwa ni kitu kinachoshangaza kwa kuwa hata mimi nilimuona mmoja wa viongozi, alikuwa Mama Juliana Matagi ya Soda. Huyu ni mwanamichezo hasa, maana alionekana ameguswa na akajitokeza.
Muda mwingi nilipokuwa msibani wakati wa kuaga, nilijaribu kutupa macho yangu huku na kule. Nilitamani sana kuwaona viongozi wa serikalini bila ya kujali ni kina nani.
Nilitamani angalau kuwaona viongozi kutoka serikali ya mkoa, ambao wangefika pale wakijua Mashali anatokea Dar es Salaam, alikuwa bondia wa kimataifa wa Tanzania na amefariki akiwa na mikanda minne ya ubingwa.
Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja naye sikumuona. Nikawa najiuliza, hivi karibuni tu aliingilia katika masuala ya mchezo wa ngumi za kulipwa na kutoa muongozo ambao hautumiki popote duniani.
Alisema alifanya vile kwa kuwa alikuwa akitetea maslahi ya mabondia, kitu ambacho si kweli. Naye hakuwepo, hakukuwa na aliyetangazwa kuwa mwakilishi wake na mwisho ikaonekana msiba huo hauwahusu watu wengi sana na huenda wengine wangejitokeza kama wangesikia msiba ni wa msanii au vinginevyo.
Kwa uwazi kabisa bila ya kuweka kona hata kidogo, haikuwa sawa ushirikiano mdogo kutoka serikalini na nimfikishie ujumbe Kiganja kwamba BMT si chombo cha kuibuka kwenye migogoro pekee.
Msiba wa Mashali bila ya kujali taarifa au hisia fulani ni mzito katika anga za michezo. BMT ni ofisi, kama angekosekana yeye, basi alitakiwa mwakilishi.
Tunajua Bunge limeanza, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye atakuwa na majukumu mazito. Vipi Kiganja ashindwe, mwenyekiti wake ashindwe, wasaidizi wengine washindwe, kwa kipi hasa kinachowafanya kuwa ‘busy’?
Siamini hata kidogo kama BMT nao wanaweza kuwa busy, huenda kuna siku watatueleza ili kuniaminisha hilo. Maana sioni wanashiriki wapi kwenye maendeleo ya michezo zaidi ya kusubiri migogoro ili waseme kama ambavyo walifanya kwenye mabadiliko ya Yanga na Simba, huku Kiganja akizungumza kauli kibao na kujipinga mwenyewe mara nyingi.
Lazima tukubali, serikali inaongozwa na watu na wanawaongoza watu. Pamoja na yote, kifo au msiba haviko kwenye katiba wala sera, lakini kama binadamu lazima tushirikiane kwenye shida na raha na ushiriki wa viongozi huongeza hamasa kwa wanawaongoza.
Niwapongeze wote walioonyesha ushirikiano wa juu wakati wa msiba huo. Hatuwezi kumhukumu Mashali, tumuachie Mungu na vyombo vya dola ambavyo vinalishughulikia suala lake.
Niendelee kukumbusha kwa viongozi wa serikali wanaohusika na michezo hasa BMT, kwamba wamefeli tena na kuonyesha hawakokaribu na wanamichezo hadi itakapoibuka migogoro, hili si jambo jema, endeleeni kujipima.
0 COMMENTS:
Post a Comment