November 23, 2016


Uongozi wa Klabu ya Simba, umetamka wazi kuwa, hautakuwa tayari timu yao kucheza mechi yoyote dhidi ya watani zao wa jadi, Yanga huku waamuzi wakiwa ni Watanzania.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara wakati akiongea na waandishi wa habari katika makao makuu ya klabu hiyo, Kariakoo jijini Dar.

Manara alisema sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kutokana na kila wanapokutana na Yanga kuonewa kwa makusudi na waamuzi ambao wanaonesha dhahiri kwamba wametumwa, hivyo wamechoka kuonewa, sasa wanataka haki itendeke kwa kuchezeshwa na waamuzi kutoka nje.

“Tumecheza na Yanga mara nyingi tu, na mchezo wetu wa mwisho wa ligi kuu tulitoka sare ya bao 1-1, lakini mwamuzi wa kati siku ile, Martin Saanya alionekana dhahiri kutunyonga.

“Matukio ni mengi ya kustaajabisha yalitokea ikiwemo kulikataa bao letu halali na kulikubali la Yanga ambalo mfungaji kabla ya kufunga, aliukumbatia mpira kama mtoto, kisha akafunga, halafu mwamuzi eti anaita kati kuashiria bao.

“Haitoshi, wachezaji wetu wanalalamika, anakuja kumuadhibu nahodha wetu, Jonas Mkude kwa kumpa kadi nyekundu ya moja kwa moja, lakini kwa kuwa Mungu hamtupi mja wake, ile kadi ikaja kufutwa na Kamati ya Saa 72 ambayo iliona mwamuzi wao kachemsha.

“Kwa hali hii, hatutakuwa radhi kuingiza timu uwanjani endapo tu waamuzi wakiwa ni walewale. Tumechoka kuonewa,” alisema Manara.

Katika kukazia hilo, Manara alisema wapo radhi wao kama Simba, mapato yote ya mchezo wao dhidi ya Yanga wagharamie kila kitu kwa waamuzi hao wa nje ili waje wasimamie haki.

“Tutagharamia kila kitu kwa ajili ya waamuzi kutoka nje, hata mapato yetu yote ya mchezo tutatoa kwani tunataka haki itendeke, mbona nchi za wenzetu kama Misri wao wanaweza kufanya hivyo kwa mechi kubwa kama yetu hii, kwa nini sisi tushindwe,” alisema.

Aidha Manara alisema kutokana na Simba kuonewa mara kwa mara, kamati ya utendaji ya klabu hiyo, imefikia makubaliano ya kumuandikia barua Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TF), Jamal Malinzi ili wakutane waongee ni kwa nini klabu yao imekuwa ikionewa kila kukicha.

“Tumemwandikia barua Malinzi ya kumtaka tukae tuzungumze tuone Simba ina tatizo gani mpaka iwe inaonewa kila siku, tunataka tulifahamu hilo ili kuondoa hali hii ambayo sasa imetuchosha,” alisema Manara na kuongeza.

“Tumeitisha mkutano wetu wa wanachama kwa ajili ya mabadiliko ya katiba, halafu tunasikia kuna mtu huyu anajiita Mohammed Kiganja (Katibu wa BMT) eti anasema kitakachoafikiwa siku hiyo wao hawakitambui wakati waziri mwenyewe amekubali.

“Sasa huyu Kiganja ni nani hasa mpaka atuendeshe kiasi hiki, sisi tunasema, katika hili hakuna wa kutuzuia, tutafanya mabadiliko ya katiba kama wanachama wakikubali, hakuna wa kutuingia katika katiba yetu hata kama serikali ilihali hatuvunji katiba ya nchi.


“Hivi kwa soka la sasa ni nani asiyependa mabadiliko, huyu Kiganja yeye amekuwa akijitokeza kwenye migogoro tu, kwa nini katika maendeleo hayupo, tumefuata sheria zote za kuitisha mkutano na tutaufanya bila ya kizuizi chochote kile,” alimaliza Manara.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic