Juzi Jumatano Simba ilipata kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Tanzania Prisons katika Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, lakini kilichotokea nyuma ya pazia kimejulikana.
Imebainika kuwa kipigo hicho ambacho ilikipata kutoka kwa Prisons kilisababishwa na wapinzani wao wa jadi, Yanga, ambao wanachuana nao vikali kuwania ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.
Mshambuliaji wa Prisons aliyeifunga Simba mabao yote hayo mawili, Victor Hangaya amesema kuwa Yanga ndiyo iliyosababisha waitungue timu hiyo juzi Jumatano.
“Kilichosababisha tukaibuka na ushindi katika mechi hiyo ni matokeo mabaya ambayo tuliyapata dhidi ya Yanga tulipocheza nao Jumapili iliyopita.
“Kipigo cha Yanga kilitufanya tuwe katika nafasi mbaya kwenye msimamo wa ligi, hivyo kwa pamoja tukakubaliana kuwa piga ua lazima tuifunge Simba ili tuweze kupanda juu kwenye msimamo huo jambo ambalo tulifanikiwa kulifanya kutokana na makosa ya safu ya ulinzi ya timu hiyo ambayo kuna wakati ilipoteza umakini,” alisema Hangaya.
Matokeo hayo yameifanya Prisons imalize mzunguko wa kwanza wa ligi kuu katika nafasi ya tisa huku ikiwa imejikusanyia pointi 19.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment