November 11, 2016Na Saleh Ally
JUMATANO Alfajiri ilikuwa ni siku ya mishituko! Maana watu wanaofuatilia masuala ya siasa, kila mmoja alikuwa akijiuliza maswali yasiyokuwa na majibu ingawa kubwa ni lile la Donald Trump ameweza vipi kushinda nafasi ya urais wa Marekani!

Kwa kuwa shughuli za uchaguzi wa Rais wa Marekani zilikamilika usiku wa kuamkia Jumatano huku wengi wakienda kulala Jumanne wakiamini kesho yake wangemshuhudia Hilary Clinton akitangazwa kuwa rais, wakaangukia kwenye kushangaa.

Maana Trump alikuwa ni mtu mpya, mfano mpya na namna gani akaonyesha ndiyo maana amefanikiwa na kuwa mfanyabiashara bilionea kwa kuwa si mtu wa kukata tamaa hata kidogo.

Kila mmoja alikuwa hamkubali, asilimia kubwa hawakuwa wakiamini atashinda. Hii ilitokana na zile kampeni zake ambazo hata mimi sikuzikubali, huenda kutokana na uwasilishaji wake wa “kikampuni”. Lakini ndiyo hivyo, ndiye Rais mpya wa Marekani.

Wakati wengine tulikuwa tunashangaa asubuhi na mapema, wapo ambao walikuwa katika wakati mgumu na walishangaa sanaa jioni ya Jumatano, safari hii ilikuwa inahusiana na mchezo wa soka.
Soka yenyewe ni Ligi Kuu Bara wakati vinara wa ligi hiyo, Simba walipoporomosha pointi nyingine tatu tena ikiwa ni mfululizo baada ya kufanya hivyo katika mechi iliyopita!

Kuna mizunguko miwili kwenye Ligi Kuu Bara, kila mmoja una mechi 15 kwa kila timu. Simba ilikuwa imecheza mechi 13 bila ya kufungwa hata moja. Kati ya hizo ilikuwa imeshinda 11, sare mbili.

Hali hii iliifanya Simba ianze kupewa nafasi ya kubeba ubingwa. Jambo ambalo nililieleza kwamba halikuwa sawasawa hata kidogo kwa kuwa tofauti ya pointi nane na Yanga, isingekuwa sahihi kuiingiza Simba kwenye ubingwa mapema hivyo.

Hesabu zangu nikaeleza, kama Simba haitafungwa hata mechi moja katika 15 za mzunguko wa kwanza, halafu ikaanza mzunguko wa pili na kushinda mechi tano mfululizo, inaweza kuwa katika nafasi ya kuanza kujipanga na ubingwa.

Lakini ilipofungwa na African Lyon kwa bao 1-0, nikawakumbusha Simba kwamba wanajichanganya wenyewe kisa kupoteza mechi moja, tena wapo waliokuwa wameanza kutupiana lawama na wamefikia wakati wa kuonyesha kwamba wao si timu inayoweza kufungwa.

Mashabiki wa Simba wamejisahau kabisa kwamba walikuwa wakifungwa hadi mechi sita katika msimu mmoja katika misimu miwili mitatu iliyopita. 

Ajabu ilikuwa ipi kufungwa mechi moja? Kipi kilichosababisha wengine kuanza kuwalaumu wachezaji, kuwaeleza kwamba hawajitumi, hawako makini mara kocha hana mbinu mbadala?

Kisa ni kufungwa mechi moja tu? Hivi Simba ina kipi hasa hadi ikifungwa iwe ajabu hadi watu wafikie kuonyesha jazba tena wengine wakitokwa na povu? Mwisho nikawaambia mnajichanganya.

Ndiyo utaona wakati wanaopenda siasa walikuwa wakishangazwa asubuhi, nyie mkashangazwa jioni kwa kuwa tayari mlishajichanganya baada ya kufungwa mechi hiyo moja ambayo mazingira yake yalionyesha kwamba nyie kufungwa ilikuwa inawezekana kabisa.
Kujichanganya nafikiri kumeichanganya zaidi Simba ambayo imepoteza mechi yake ya pili ndani ya wiki moja, tena zikiwa ni mechi zinazofuatana baada ya kucheza mechi 13 bila ya kufungwa.

Hili halikuwa jambo zuri kwa Simba hata kama mtajaribu kulikwepa. Lilikuwa jambo lililotokana na mambo mawili. Kwanza mambo ya mpira na pili kujitakia, jifunzeni.
Mechi ya Lyon, yalikuwa masuala ya mpira na soka linapendwa kwa kuwa lina mambo yake mengine ni ‘sapraiz’. Lakini suala la pili la kufungwa na Prisons ni kujitakia kutokana na kujijaza presha na kujichanganya wenyewe.

Mzunguko wa pili, nao utaanza na kuna mechi 15. Simba ina kazi mpya ya kujenga tena hali ya kujiamini ambayo ingekuwa bora kama wangemaliza nayo. 

Lakini kwa wale waliohusika na kujichanganya wenyewe, basi huu ni wakati mwafaka wa kujifunza kwamba katika soka kuna mambo yake na hayalazimishwi kubadilishwa, ukifanya hivyo, unajichanganya.

SOURCE: CHAMPIONI0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV