November 23, 2016Klabu ya Yanga imetenga kitita cha shilingi milioni 50 kuwasajili viungo nyota wawili wa Mbeya City ili kutibu tatizo linalowasibu kwa sasa.

Yanga inataka kuwasajili nyota hao ikiwa ni njia ya kukifanyia marekebisho kikosi chao kinachojiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Nyota hao wa Mbeya City wanaowaniwa na Yanga ni Raphael Alpha na Kenny Ally ambaye aliifunga timu hiyo bao la pili wakati walipokutana katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi kuu kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya ambapo Yanga ilifungwa 2-1.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya Kamati ya Usajili ya Yanga, nyota hao kila mmoja atapewa shilingi milioni 25 kati ya milioni 50 zilizotengwa.

Chanzo hicho kilisema fedha hizo watapatiwa baada ya mazungumzo ya awali waliyofanya na wachezaji hao hivi karibuni.

“Tumefikia muafaka mzuri na Kenny na Alpha katika kukubaliana kuingia mkataba nao wa miaka miwili, lakini kizuizi chetu kinachosababisha tusimalizane haraka ni kutokana na timu zinazowamiliki kudai zina mikataba nao.

“Wakati Mbeya City wakidai wana mikataba, wachezaji wenyewe wanasema mikataba imemalizika, hivyo bado tupo njia panda,” kilisema chanzo hicho.


Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit kwa njia ya simu ili kuzungumzia hilo, simu yake iliita bila kupokelewa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV