Na Saleh Ally
KILA mmoja anaweza kuwa na uamuzi wake wa kufanya yale ambayo anaamini ni sahihi kulingana na kile ambacho amepanga kukifanya.
Uongozi wa Klabu ya Simba umeamua kufanya marekebisho ambayo kwa asilimia fulani ninaweza kuyaita ni makubwa katika kikosi chake katika mechi 15 zijazo za Ligi Kuu Bara na zile za Kombe la FA.
Simba imekuwa katika mjadala mkubwa wa kuwaacha wachezaji kadhaa akiwemo kipa Vincent Angban raia wa Ivory Coast ambaye ni kipa wangu bora kwa mzunguko wa kwanza.
Aliiongoza Simba kushinda mechi 11 za Ligi Kuu Bara mzunguko wa kwanza, sare mbili na ikapoteza mbili za mwisho katika mzunguko huo, moja ikiwa nyumbani dhidi ya African Lyon na ya pili mjini Mbeya dhidi ya Prisons.
Simba wameona kipa huyo hafai na mwisho wamemsajili kipa Daniel Agyei kutoka Ghana ambaye aliichezea Medeama kwa mafanikio makubwa sana msimu uliopita, hasa ikiwa inashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Bado Simba haijatangaza, lakini iliamua kufanya uamuzi wa kuachana na kipa mmoja wa kigeni ikiwezekana kwa lengo zuri kabisa la kuwapa nafasi vijana wa Kitanzania kama Peter Manyika na Denis Richard wakue kimpira.
Wazo hilo la Simba ni bora kabisa kuliko wangekuwa na makipa wawili wote kutoka nje ya Tanzania. Kwa kiwango cha mpira wa hapa nyumbani na hata Simba yenyewe, lisingekuwa jambo sahihi hata kidogo kuwa nao wote.
Kama utazungumzia nafasi ya hawa makipa wawili, kitaalamu unaona Simba haikuwa sahihi hata kidogo na imekuwa ikihangaika bila ya sababu za msingi kwani kama utatumia hesabu za mpira, hakuna sehemu Simba inalindwa kuonyesha ilikuwa sahihi.
Safu ya ushambuliaji ya Simba ilifunga mabao 26 katika mechi 15, ikafungwa mabao sita tu. Utaona kiasi gani safu ya ulinzi ya kikosi hicho ambayo iliongozwa na Angban ilifanya kazi nzuri kabisa.
Nasema kazi nzuri kwa kuwa katika mechi 15 za mzunguko wa kwanza, Simba ndiyo imefungwa mabao machache zaidi kuliko timu zingine kwani baada ya yenyewe iliyofungwa mabao sita tu, inafuatiwa na Yanga iliyofungwa mabao nane, Prisons 10, Stand 12 na Azam FC 14.
Sasa unaweza vipi kumuondoa kiongozi wa ubora wa ulinzi? Hili ndilo jambo ambalo linanipa ugumu kidogo hasa kama utazungumzia kigezo walichotumia Simba. Labda kama kuna jambo waligundua wakalisoma na kulifanyia kazi katika zile mechi mbili walizopoteza na wanaweza kusema lilikuwa si la kawaida.
Ikiwa watazungumzia mambo kwa hesabu za mpira ambazo zinaendeshwa na hesabu, hakika itakuwa ni moja ya mambo ya ajabu wamefanya na wanaweza kulindwa na mafanikio ya Agyei pekee.
Agyei ni kipa mzuri kwa namna tulivyomuona akiitumikia Medeama, lakini lazima tukubali, hapa ni Tanzania na si Ghana, hivyo kuna mambo kadhaa anatakiwa kuzoea kama mazingira ya viwanja na mambo mengine.
Moja ya mambo makubwa kabisa ni aina ya uchezaji kati yake na wachezaji wengine wa Simba, hasa kwenye safu ya ulinzi katika ule mfumo wa ujengaji timu, nani ana makosa haya, nini cha kumsaidia na nini cha kufanya wakati fulani ili kuungana na wengine na kuwa kitu kimoja.
Kama unakumbuka uchezaji wa Angban, alionekana ameizoea Simba, anajua nini cha kufanya kulingana na wakati fulani jambo ambalo hata kama Agyei ni mzuri vipi, bado atahitaji muda.
Simba watalazimika kushukuru kama watakwenda na kushinda mechi mbili mfululizo, hali inayoweza kumjengea kujiamini kwa Mghana huyo. Kama isipokuwa hivyo, inaweza kuwa shida.
Hivyo Simba ni kama wamecheza patapotea na wanalazimika kuomba iwe pata na si potea kwa kuwa nafasi ya kipa, si ya kuchezeachezea. Maana yake, pia tunaweza kujifunza katika hili, tusubiri.







uchambuzi wako umesahau kwamba UKUTA nao ulichangia sana kuinusuru simba na kapu la magoli na pia ukweli kwamba Golikipa kama mtu wa mwisho anategemewa kuwa msaada wa mwisho pia kitu ambacho Vice alishindwa kwa nyakati kadhaaa...........muhimu ulichosema ni kwamba isingalikua vyema kuwa na makipa wawili wa kimataifa thus kutowapa wazawa nafasi
ReplyDeleteTatizo hawa wazawa hawajielewi na tukiwategemea sana wazawa hatutafika mbalimi nafikiri usajili wa simba umezingatia matakwa ya kocha na anaogopa kuwatumia wazawa wasije wakamharibia kazi yake bureee
ReplyDeleteNakubaliana na wewe mia kwa mia.
ReplyDeleteMpira unaongozwa na takwimu na hakuna siasa.
Sijasikia sehemu yoyote duniani kipa wa timu inayoongoza ligi, inayoongoza kwa kufungwa magoli machache, kipa mwenye clean sheet nyingi eti anafukuzwa kuwa ni mbovu, katikati ya ligi.
Hoja kuwa eti amekua akilindwa na bekini za kijinga, maana hizo clean sheet alizipataje ?
Lakini wengine hatushangai, si hawa hawa walimuuza Tambwe, mfungaji bora kuwa eti hakabi na anavizia tu !! Matokeo yake tunayajua.. (sijui kazi ya mfungaji ni nini na hawa viongozi wamecheza mpira au mchezo gani.
Si hawa hawa walifukuza makocha katikati ya ligi, kisa hatoi mazoezi magumu, au anasherekea siku za kuzaliwa na wachezaji lkn timu ilikuwa inashinda!!
Hayo yote miaka 4 hakuna mafanikio wala kombe, na mwaka huu, unabadili timu ya ushindi katikati ya ligi sitegemei lolote jipya !!
Tunahitaji watu wanaojua mpira kuwa viongozi ili mpira wetu ukue.