Kocha wa Simba, Joseph Omog amekubali yaishe kwa beki wake Juuko Murshid na hamtegemei tena kikosini badala yake amempa majukumu yote Abdi Banda aliyekuwa hana nafasi kikosini.
Juuko yupo kwao Uganda na kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo, The Cranes ambacho kitashiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwakani huko Gabon.
Omog raia wa Cameroon anaamini chini ya ukuta wa mabeki wa kati, Banda na Method Mwanjale timu yake haitafungwa mabao ya ajabu kama ilivyokuwa katika mzunguko wa kwanza.
Omog alisema safu yake ya ulinzi aliyoifanyia mabadiliko hivi karibuni kwa kumpatia nafasi ya kucheza mchezaji wake kiraka, Banda kama beki wa kati akishirikiana na Mwanjale inafanya vizuri.
Alisema Banda anafanya majukumu makubwa ambayo hapo awali walinzi wa kati wa timu hiyo walikuwa hawayafanyi kama vile kucheza mpira yote ya vichwa na ile ya chini kwa ustadi mkubwa.
“Baada ya kutokuwa na Juuko kulikuwa na tatizo la umakini lakini sasa baada ya kumpatia nafasi Banda naona umakini umeongezeka na anafanya vizuri zaidi kwa kucheza mipira ya vichwa ambayo ilikuwa ni tatizo kubwa kwetu.
“Kutokana na hali hiyo, sasa sitegemei kuona tunafungwa mabao ya ajabu lakini pia hivi sasa najitahidi sana kuhakikisha safu yetu ya ushambuliaji nayo inakuwa moto wa kuotea mbali,” alisema Omog.







0 COMMENTS:
Post a Comment