January 14, 2017
Siku chache baada ya ile ishu yake ya kutaka kucheza soka la kulipwa nchini Misri imekwama, straika wa Simba, Ibrahim Ajibu amesema kwa sasa hajui nini afanye na hana uhakika kama atasaini mkataba mpya katika timu yake.

Ajibu ambaye mwishoni mwa mwaka jana alikwenda Misri kufanya majaribio kwenye timu ya Haras El Hadood, licha ya kufuzu lakini alishindwa kujiunga na timu hiyo kutokana na dirisha la usajili kufungwa kabla timu hiyo haijamalizana na Simba.

Aidha, hivi karibuni kulikuwa na mvutano mkubwa juu ya mshambuliaji huyo kuongeza mkataba mwingine wa kuitumikia Simba kwa madai kuwa anasubiria ule wa awali ufikie tamati kwanza.

Ajibu alisema hadi sasa hajui iwapo atasaini mkataba mpya Simba ama la kwa kuwa kuna mipango mingine anayoendelea kuifanya kwa sasa chini ya meneja wake.

“Sielewi kama nitaongeza mkataba mwingine Simba ama la, siwezi kuweka wazi vitu vyangu kwa kuwa kuna mipango ambayo naendelea kuipanga chini ya meneja wangu ambaye kuna vitu anafuatilia kwa sasa.

“Sifahamu kuhusu suala langu la kule nilipokwenda limefikia wapi na anayejua kila kitu kwa sasa ni meneja wangu ambaye ndiye anayefuatilia kuhusu mambo yangu na Mungu akipenda kila kitu nitakiweka wazi,” alisema Ajibu.

Simba mara kadhaa imekuwa ikisisitiza kuwa Ajibu ni mchezaji wao na mambo yote kuhusu mkataba mpya ni siri kati yao na mshambuliaji huyo.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV