January 24, 2017
Nahodha wa Simba, Jonas Mkude amelalamika kulishwa maneno akisema kuna mtandao unaomsakama akionyesha hofu huenda kuna watu wanataka kuvivuruga Simba.

Katika taarifa yake iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Simba, Mkude amesema suala la kusema yeye analalamikia mshahara halina ukweli wowote.

"Jana usiku nilitumiwa taarifa ya upotoshwaji iliosambazwa na mtandao unaojiita Goal, eti wachezaji Simba wanadai mishahara ya miezi miwili," alisema.

"Taarifa hiyo imesema mshahara ni chanzo cha timu kutofanya vizuri. Napenda kuwaarifu wanachama na washabiki wetu kuwa, taarifa hizo zinalenga kutuondoa katika nia yetu ya kuipa ubingwa Simba.

"Kwa maana ya weledi wa uandishi, hilo si sahihi na si jambo jema," alisisitiza.

"Naomba tushikamane na kuamini tunafanya vema, timu inayoongoza ligi na iliyofuzu kwenye raundi nyingine utasemaje inafanya vibaya," alihoji. 

Simba ndiyo kinara wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 45 wakifuatiwa kwa karibu na Yanga wenye pointi 43.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV