January 20, 2017
LONDON, England
WAKATI klabu nyingi kubwa za Ulaya zikisifika kuwa na matumizi makubwa ya fedha hasa wakati wa usajili, imebainika kuwa kumbe Tottenham Hotspur ina wastani mzuri wa kuuza na kununua wachezaji tofauti na vigogo wengine.

Utafiti uliofanywa kwa klabu kubwa katika mauzo yao tangu msimu wa mwaka 2012-13 hadi sasa ikiwa ni misimu mitano imepita, inaonekana kuna klabu nyingi zimeingia hasara ya kutumia fedha nyingi ndani ya miaka mitano.

Zifuatazo ni takwimu za matumizi ya klabu hizo kwa jinsi zilivyonunua na kuuza wachezaji ndani ya miaka mitano iliyopita katika Ligi Kuu ya England ‘Premier League’.

MANCHESTER CITY
Imetumia jumla ya pauni milioni 565.65 kufanya usajili tangu msimu wa 2012-13 na kuwa klabu ambayo imetoa kiasi kikubwa cha fedha kusajili kuliko zote England.

Baadhi ya waliosajiliwa kwa dau kubwa klabuni hapo ni John Stones pauni 47.5m, Kevin De Bruyne pauni 55m, Leroy Sane pauni 37m na Raheem Sterling pauni 45m.

Kwa muda wote huo kiwango chao walichotumia kuuza wachezaji ni pauni 163.1m, hivyo kuwa na wastani wa kutumia pauni 402.55m kwa muda huo ukilinganisha kiwango walichotoa na walichopokea.

Kununua: Pauni 565.65m
Kuuza: Pauni 163.1m
Kilichotumika: Pauni 402.55m


MANCHESTER UNITED
Chini ya uongozi wa Ed Woodward, klabu hii nayo imeingia kwenye orodha ya klabu zilizotumia fedha nyingi katika usajili, zaidi ya pauni milioni 500.

Msimu huu tu pekee iliweka rekodi ya kumsajili Paul Pogba kwa pauni milioni 89 na kuwa mchezaji ghali zaidi duniani akitokea Juventus. 

Wengine waliotua hapa ni Eric Bailly kwa pauni 30m na Henrikh Mkhitaryan pauni 30m.

Akizungumzia tabia ya klabu yake kutumia fedha nyingi, Kocha Jose Mourinho anasema United ni klabu kubwa na suala hilo ni kawaida.

Kununua: Pauni 528.8m
Kuuza: Pauni 160.15m
Kilichotumika: Pauni 368.65m


ARSENAL
Awali haikuwemo kwenye orodha ya klabu zinazotumia fedha nyingi kusajili lakini miaka ya hivi karibuni iliamua kufungua pochi na kumwaga fedha.

Ujio wa Mesut Ozil mwaka 2013 kwa pauni 42.5m pamoja na Alexis Sanchez kwa pauni 35m mwaka 2014, uliongeza nguvu ya timu hiyo kutumia fedha nyingi.

Msimu huu pia ikawaongeza Granit Xhaka na Shkodran Mustafi, hivyo kuifanya iwe na nguvu katika klabu zinazotoa fedha England.

Kununua: Pauni 298.34m
Kuuza: Pauni 92.45m
Kilichotumika: Pauni 205.89m 


CHELSEA
Bilionea wa klabu hii, Roman Abramovich amekuwa akisifika kwa kumwaga fedha lakini miaka ya hivi karibuni klabu yake imekuwa vizuri katika kuuza kwa bei kubwa.

Oscar kwenda Shanghai SIPG kwa pauni 52m ni mfano wa jinsi walivyo safi katika mauzo, hali hiyo imepunguza makali ya kutumia fedha nyingi kusajili.

Kununua: Pauni 507.45m
Kuuza: Pauni 315.15m
Kilichotumika: Pauni 192.3m 


LIVERPOOL
Sadio Mane alisajiliwa kwa pauni 34m, Roberto Firmino pauni 29m, Georginio Wijnaldum pauni 25m, Adam Lallana pauni 25m, hao wote wanaifanya Liverpool kuwa wanunuaji wazuri kwa bei kubwa.

Pamoja na hivyo, bado katika suala la mauzo klabu hiyo nayo imekuwa vizuri ili kubalansi akaunti zao za benki.

Kununua: Pauni 365.6m
Kuuza: Pauni 244.08m
Kilichotumika: Pauni 121.52m


TOTTENHAM
Inaweza kuwashangaza wengi lakini huo ndiyo uhalisia, kitendo cha kumuuza Gareth Bale kwenda Real Madrid mwaka 2013 kwa pauni 85m, kiliweka sawa akaunti zao za benki na kuwafanya kuwa na nguvu ya kutumia fedha kusajili wachezaji wengine.

Wapo kwenye mchakato wa kujenga uwanja wao mpya kwa pauni 750m, hivyo lazima wabane matumizi. Kama ambavyo Rais wa Tanzania, John Magufuli anavyosisitiza kubana matumizi, ndivyo Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy ambavyo amekuwa akisisitiza hivyo klabuni kwake.

Kununua: Pauni 315.45m
Kuuza: Pauni 314.45m

Kilichotumika: Pauni 1m

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV