Katika kuhakikisha wanafanikiwa kuibuka na ushindi katika mchezo wa Jumamosi wa watani wa jadi, Kocha wa Yanga, George Lwandamina, ameonekana kuwapa jukumu washambuliaji wake la kuhakikisha wanafanikiwa kufumania nyavu katika mchezo huo.
Kocha huyo juzi na jana alikuwa anapambana na washambuliaji wake Amissi Tambwe na Simon Msuva kwenye mazoezi akiwafundisha mbinu mbalimbali za kufunga mabao.
Yanga ambayo imeweka kambi yake Kigamboni na kufanya mazoezi yake katika Uwanja wa Polisi, inatarajia kukutana na Simba, Jumamosi katika mchezo wa mzunguko wa pili wa ligi kuu ambapo mchezo wa awali timu hizo zilipokutana matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1.
Chanzo kutoka benchi la ufundi la Yanga, kilieleza kuwa, Lwandamina kwa sasa yupo katika kazi moja tu ya kuwapatia mafunzo maalumu washambuliaji kuhakikisha wanafanikiwa kufanya vizuri na kufumania nyavu katika mchezo wa Jumamosi.
“Tunaendelea vizuri na kambi yetu ambayo ipo Kigamboni na tunafanya mazoezi katika Uwanja wa Polisi na muda huu ndiyo tumetoka mazoezini, kikosi kizima kipo vizuri kuelekea mchezo huo.
“Mwalimu anaonekana kuwa makini zaidi katika kuhakikisha safu ya ushambuliaji inakuwa nzuri zaidi kwa kupunguza ubutu na ndiyo sehemu anayoikazania kwa sasa kwa kuhakikisha washambuliaji wanafanya vizuri siku ya Jumamosi, kwani muda mwingi amekuwa akiwafundisha wao,” kilisema chanzo hicho.
SOURCE: CHAMPIONI (USIKOSE LIKO MTAANI LEO JUMATANO)
0 COMMENTS:
Post a Comment