February 22, 2017Huku zikiwa zimebaki siku tatu pekee kabla ya pambano baina ya Simba na Yanga, Kocha Msaidizi wa Simba, Mganda, Jackson Mayanja, amesema kikosi chao kipo imara na kamwe hawaogopi Yanga kutokana na uwezo wao baada ya kupata matokeo mazuri kwenye mechi za hivi karibuni, tena kwa mabao mengi.

Simba watakuwa wenyeji wa Yanga kwenye pambano la ‘Kariakoo Derby’ litakalopigwa wikiendi hii katika Uwanja wa Taifa, Dar ambapo Simba watashuka dimbani wakiwa ndiyo vinara wa ligi wakiwa na pointi 51.

Mayanja amesema pamoja na watu kuiona mechi hiyo kuwa kubwa na ngumu lakini kwao wanaupa mchezo huo nafasi ya kawaida kama wanavyocheza na timu nyingine, hivyo hawana sababu ya kuogopa na badala yake watapambana kuweza kupata ushindi.

“Matokeo ya mechi za Majimaji, Prisons na African Lyon yanatupa matumaini mazuri ya kushinda mechi dhidi ya Yanga kwa sababu vijana walicheza kwa hali ya juu na walipambana na hali hiyo tunaamini itaendelea hata mechi hii.

“Lakini kingine sisi tunachukulia mchezo huu kama mechi za kawaida tu tofauti na wengine wanavyoona eti ni mechi kubwa, lakini kikubwa tutapambana kushinda ili tuweze kuongeza gepu la pointi baina yetu na Yanga ambao wanashika nafasi ya pili,” alisema Mayanja.


SOURCE: CHAMPIONI (USIKOSE LIKO MTAANI LEO JUMATANO)

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV